Wednesday, August 20, 2014

LUIS FIGO KUONGOZA MSAFARA WA KWANZA WA MAGWIJI WA REAL MADRID KUTUA NCHINI KESHO


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MSAFARA wa kwanza wa magwiji wa Real Madrid, ‘Real Madrid Legends’ utatua nchini Tanzania kesho, ukitarajiwa kuongozwa na mwanasoka bora wa zamani wa dunia na Ulaya, Mreno, Luis Filipe Madeira Figo.
Magwiji hao watashuka dimbani jumamosi Agosti 23 dhidi ya kikosi maalumu cha nyota wa zamani wa Tanzania ‘Tanzania All Stars’ ndani ya uwanja wa kisasa wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Figo ataongozana na nyota wengine wawili waliotamba na Real Madrid miaka ya nyuma, Muingereza Michael Owen na Christian Karembeu.
Figo aliyestaafu soka mwaka 2009, alishinda tuzo mbili mfululizo mwaka 2000 ambazo mwanasoka bora wa Ulya na Dunia na katika enzi zake za kucheza soka alikuwa mchezaji hatari kupita maelezo na sasa anakuja kukumbushia ufundi wake katika ardhi ya Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na Figo, mwanasoka mwingine bora wa zamani wa dunia, Zinedine Zidane na Mbrazil Ronaldo de Lima wanatarajia kutua nchini Ijumaa na kundi kubwa la magwiji hao.
Mkurugenzi wa makampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN) (waandaaji wa ziara hiyo), Farough Baghozah amekaririwa akisema mapokezi makubwa kwa ajili ya magwiji hao yameandaliwa na watawasili kwa mafungu, lakini kundi kubwa litaingia nchini Agosti 22.
Baghozah alisema magwiji hao watapokelewa kwa maandamano kutoka uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam na kupelekwa hoteli ya Ladger Plaza, Bahari Beach.
Tayari kikosi cha ‘Tanzania All Stars’ kimeanza mazoezi katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam chini ya kocha maarufu, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’akisaidiwa na Fredy Felix Minziro na Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’.
Mlinda mlango na nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Mwamweja ametoa wito wa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwaona nyota wao wa zamani kwasababu wamejipanga vizuri.
 Mwamweja alikiri kuwa wamekaa muda mrefu bila kucheza mpira, lakini mazoezi hayo yamewaongezea nguvu ya kucheza mechi hiyo.
Kipa huyo anayetarajia kuanza katika kikosi cha kwanza alisema watajifunza mengi kutoka kwa magwiji hao, lakini nao watajifunza vitu fulani kutoka kwa wachezaji wa Tanzania.
Wachezaji wanaoendelea kujifua kwa ajili ya kukumbushia enzi zao na magwiji wa Real Madrid ni:
Makipa waliowahi kutamba nchini Tanzania, Mohamed Mwameja na Peter Manyika.
Watakaosuka safu ya ulinzi ni mabeki Shadrack John Nsajigwa Mwandemele, Boniface Pawasa, John Mwansasu,  Mecky Mexime, Abubakar Kombo, George Masatu na Habib Kondo, 
Viungo ni:  Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’, Shaaban Ramadhani, Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’, Yussuf Macho Musso, Abdul Mashine, Abdul Maneno, Mao Mkami, Steven Nyenge, Akida Makunda na Mtwa Kihwelo.

Washambuliaji: Monja Liseki, Iddi Moshi, Dua Said, Emmanuel Gabriel Mwakyusa, Said Maulid ‘SMG’, Thomas Kipese, Nasor Mwinyi ‘Bwanga’, Edibilly Lunyamila, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Clement Kahbuka, Madaraka Suleiman ‘Mzee wa Kiminyio’ na Akida Makunda.

No comments:

Post a Comment