Tuesday, August 19, 2014

HARUNA SHAMTE,JABIR AZIZ NA JACKSON CHOVE WASANI JKT RUVU


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MAAFANDE wa JKT Ruvu wamekamilisha usajili wa wachezaji watatu kati ya wengi waliokuwa wanafanya majaribio chini ya kocha mkuu, Fredy Felix Minziro.
Beki wa kulia aliyeichezea Simba sc msimu uliopita, Haruna Ramadhan Shamte amesajiliwa na maafane hao na kusaini mkataba mwa mwaka mmoja.
Pia nyota wa zamani wa Simba sc na Azam fc, Jabir Aziz ‘Stima’ ameanguka mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo yenye nia ya kuonesha changamoto kubwa zaidi msimu ujao.
Katika kuhakikisha lango lake linakuwa mikono salama, klabu hiyo imemsainisha mlinda mlango mzoefu, Jackson Chove mkataba wa mwaka mmoja.
Wachezaji hao watatu walikuwa chini ya uangalizi wa kocha Minziro kwa muda mrefu kwa lengo la kujiridhisha na viwango vyao pamoja na suala muhimu la nidhamu.
Jabir Aziz 'Stima'

Wachezaji wengine waliokuwa wanafanya majaribio na klabu hiyo ni pamoja na Betram Mombeki na Henry Joseph, wote waliachwa na Simba sc mwishoni mwa msimu uliopita.
Pia Athumani Idd ‘Chuji’ alijitokeza mara kadhaa katika mazoezi hayo, lakini aliondoka zake baadaye na sasa anajifua na Mwadui FC ya Shinyanga inayoshiriki ligi daraja la kwanza.
Meneja wa JKT Ruvu, Frank Joel Cibaya aliwahi kukaririwa na mtandao huu akisema wachezaji wengi walioachwa na klabu kubwa za Simba na Yanga wanaomba kufanya majaribio klabuni hapo, lakini kocha Minziro yuko makini zaidi kuangalia nani anamfaa.
Jackson Chove

Cibaya alimtaja Aziz, Shamte na Chove kuwa walionesha juhudi kubwa kwa muda wote wa uangalizi, hivyo kocha amependekeza wasajiliwe rasmi kuitumikia klabu hiyo.
Meneja huyo alisema wachezaji wengi wanaotoka timu kubwa huwa wanasumbua sana wanapojiunga na timu ndogo wakitaka kupata kila kitu walichokuwa wanapata Simba na Yanga.

Dirisha la usajili limeongezwa kwa siku 10  hadi Agosti 27 mwaka huu, hivyo bado maafande wana nafasi ya kuongeza au kupunguza wachezaji wanaoona hawana manufaa kwao.

No comments:

Post a Comment