Spika wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) Dk. Margaret Nantongo Zziwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es Salaam leo juu ya mkutano wa kwanza wa Bunge la tatu unaotaraji kuanza kesho katika ukumbi wa Karimjee na kufunguliwa na Rais Jakaya Kikwete kesho kutwa.
Spika wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) Dk. Margaret Nantongo Zziwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es Salaam jana juu ya mkutano wa kwanza wa Bunge la tatu unaofanyika ukumbi wa Karimjee. Wengine kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Amantius Msole, wabunge wa EALA kutoka Tanzania Twaha Taslima na Shy Rose Banji
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Wabunge kutoka Tanzania, Adam Kimbisa, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es Salaam leo, juu ya mkutano wa kwanza wa Bunge la tatu unaofanyika ukumbi wa Karimjee. Kushoto ni Spika wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) Dk. Margaret Nantongo Zziwa,wabunge wa EALA kutoka Tanzania, Twaha Taslima na Shy Rose Banji.
Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Twaha Taslima akizungumza na wabunge wenzake.
Mkutano ukiendelea
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Amantius Msole akifafanua jambo. Kulia ni Spika wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA) Dk. Margaret Nantongo Zziwa
Wanahabari wakichukua dondoo za mkutano huo.
Mbunge Shy Rose Banji akifafanua jambo
Wabunge wakibadilishana mawazo baada ya kumaliza kwa mkutano huo ambapo walisifu kupata idadi kubwa ya waandishi kuliko nchi nyingine.
Ofisa wa Bunge la Tanzania Prosper Minja (katikati) akizungumza jambo na Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki Adam Kimbisa (kulia) na Angela Kiziga.
Wabunge wakitoka nje ya chumba cha mkutano.
********
MKUTANO WA KWANZA – KIKAO CHA TATU – BUNGE LA TATU
(IMETOLEWA NA MH. (Dk.) MARGARET NANTONGO ZZIWA – SPIKA, EALA)
Ndugu Waandishi wa Habari,
Napenda kuwakaribisha wote kwenye mkutano huu wa waandishi wa habari ulioitishwa ili kuwafahamisha kuhusu mkutano wa kwanza wa kikao cha tatu cha Bunge la Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) unaonza tarehe 27 Agosti 2014 mpaka tarehe 5 Septemba 2014 kwenye ukumbi wa Karimjee hapa jijini Dar es Salaam.
Kwa niaba ya Bunge la EALA na kwa niaba yangu mimi binafsi, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, na Serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukubali kuwa mwenyeji wa EALA kwenye nchi hii kubwa na kwa kukubali kutufungulia rasmi mkutano wetu.
Tunatoa shukrani za pekee kwa uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dk. Kikwete kwa nchi ya Tanzania na vilevile kwa mchango wake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama mwanachama wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hii (Summit).
Hii ni mara ya kwanza kwa Bunge la Tatu kufanya mkutano wake Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wetu mahsusi tuliojiwekea wa kufanya vikao kwa zamu kwenye nchi zote wanachama ili kuliweka Bunge hili liwe karibu zaidi na wananchi ili wapate fursa kufahamu kuhusu shughuli za EALA. Vikao vya Bunge hili sasa hufanyika mara kwa mara kwenye nchi wanachama kwa mujibu wa Ibara ya 55 ya Mkataba (Treaty) wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tunapenda kumshukuru mwenyeji wetu, Spika wa Bunge la Tanzania, Mh. Anna Makinda, kwa kutupa nafasi ya kutumia nyenzo za Bunge la Tanzania na ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya mkutano wetu. Hii inaendelea kudhihirisha uwepo wa mahusiano ya karibu ya kikazi kati ya Bunge la Tanzania na EALA.
Katika kipindi kijacho cha wiki mbili, ratiba ya shughuli za kazi za Bunge la EALA ni kama ifuatavyo:
· Ufunguzi rasmi wa mkutano wa Bunge na Mh. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete;
· Kupokea na kujadili ripoti kutoka Kamati mbalimbali za Bunge. Ripoti hizi ni pamoja na ya Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Upatanishi wa Migogoro (Committee on Regional Affairs and Conflict Resolutions) and Kituo cha Uongozi cha Afrika cha Taasisi za Afrika Mashariki na Usalama wa Jumuiya (African Leadership Centre on East African Societies and Regional Security); Ripoti ya Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili (Committee on Agriculture, Tourism and Natural Resources) kuhusu semina ya Wabunge wa Jumuiya juu ya Misitu na Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Ripoti ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (Committee on Communication, Trade and Investment) kuhusu Sekta ya Urafiri wa Anga ya EAC.
· Aidha, kuna Miswada kadhaa ambayo iko mbele ya Kamati mbalimbali za Bunge. Hii ni pamoja na:
a) Muswada wa Elimu -- the EAC Integration (Education) Bill – ambapo Bunge linatarajia kupokea taarifa kutoka Kamati ya Masuala ya Jumuiya na Upatanishi wa Migogoro (Committee on Regional Affairs and Conflict Resolution) kuhusu hatua waliofikia;
b) Muswada wa Masuala ya Ushirika -- the EAC Co-operatives Societies Bill – huu uko mbele ya Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili (Committee on Agriculture, Tourism and Natural Resources), ambayo hivi karibuni inatarajiwa kuanza vikao vya wazi;
c) Muswada wa Masuala ya Biashara -- the EAC Joint Trade Negotiations (Repeal) Bill – ambao uko mbele ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (Committee on Communication, Trade and Investments).
· Hatimaye, Bunge la EALA litapitia Hoja, Maazimio na Maswali mbalimbali ambayo yatakuwa yameletwa kwenye mkutano.
Kwa ujumla, EALA inatoa mchango wake kwenye mchakato wa utengamano kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na mfumo rasmi wa kisheria na usimamizi ili kuwepo na kipaumbele kwa ajenda ya utengamano.
Ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wa Afrika Mashariki wanahusishwa kwenye mchakato huu. Kama EALA tutaendelea kuwa karibu na wananchi wa Jumuiya hii na kuhakikisha kuwa maoni yao yanasikilizwa wakati wa kutunga Sheria.
Siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, EALA ilifanya ziara mahsusi kwenye vyombo vya habari vya IPP Media jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni hayo, Dk. Reginald Mengi. Tunapenda kutoa shukrani kwa IPP Media kwa kuamua kutuunga mkono kwenye urushwaji wa moja kwa moja (live broadcast) wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa Bunge letu. Hii ni hatua ya kwanza ya jitihada zetu za kuhakikisha kuwa tunajenga mahusiano ya karibu kati ya vyombo vya habari na Wabunge wa EALA ili tuweze kutangaza ajenda ya utengamano na kuelimisha wananchi kuhusu majukumu ya Bunge letu. Tutaendelea kufanya majadiliano haya na vyombo vya habari vingine kwenye nchi zote wanachana wa EAC.
Taasisi nyingine ambazo tutazitembelea wakati wa kikao chetu ni pamoja na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) mnamo tarehe 29 Agosti 2014, na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TASUBA) iliyopo Bagamoyo tarehe 30 Agosti 2014. Ziara hizi zinatarajia kuongeza ushirikiano kati ya EALA na washikadau husika kwa upande mmoja na kuboresha kazi zetu za utungaji wa sheria kwa upande mwingine.
Jumuiya ya EAC hivi sasa inapitia katika kipindi muhimu cha mchakato wa utengamano. Tunatoa pongezi kwa nchi zote wanachama kwa kuonesha moyo wa dhati wa kuimarisha mchakato wa utengamano kwa kutekeleza Itifaki mbalimbali.
Umoja wa Forodha (Customs Union) sasa uko kwenye hatua nzuri ya utekelezaji. Ndani ya umoja huu, bidhaa zinazozalishwa kwenye Jumuiya hazitozwi kodi na nchi wanachama na zinafaidika na kodi sawasawa ya nje, pamoja na utaratibu na nyaraka za pamoja. Kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory) ni jambo jingine kubwa kwenye EAC, kwani kutawezesha bidhaa ziweze kusafiri kwa kasi zaidi. Lengo la kuwa na Himaya Moja ya Forodha ni kuhakikisha kuwa nchi wanachana zinanufaika kwa pamoja kwa kuunganisha uchumi wa nchi hizi kwa lengo la kuunga mkono jitihada za maendeleo ya uchumi.
Mwaka wa nne wa utekelezaji wa Soko la Pamoja umeanza. Itifaki ya Soko la Pamoja (Common Market Protocol) inahakikisha kuwa kunakuwa hakuna vikwazo vyovyote kwa bidhaa, huduma, ajira, mitaji na uanzishaji wa biashara miongoni mwa wananchi wa nchi wanachana wa Jumuiya. Kwa ujumla, nchi wanachama zimeonesha utashi mkubwa wa kusimamia utekelezaji wa Itifaki hii. Jumuiya ya EAC pia imesaini Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha (Monetary Union), ambayo ni hatua ya tatu muhimu kwenye mchakato wa utengemano ambao unapitia kwenye hatua kubwa nne.
Nimetaarifiwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshatia saini kupitisha Itifaki ya Umoja wa Fedha (Monetary Union Protocol).
Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha unatarajia kuanza mara baada ya nchi zote wanachama kuidhinisha itifaki hiyo na kukabidhi nyaraka hizo kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa EAC. Hii ni hatua muhimu sana ambayo itasimika mchakato huu wa utengamano. Hata hivyo, utekelezaji rasmi wa Itifaki hii utahitaji kuwepo kwa sheria mbalimbali. Kama EALA, tumejidhatiti kuhakikisha kuwa tunatunga sheria hizi na hapa tungependa kutoa wito kwa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Council of Ministers) kuleta hii Miswada kwenye Bunge haraka iwezekanavyo.
Pamoja na hatua hizi kubwa ambazo tumepiga, bado kuna changamoto. Kama ilivyoelezwa awali, hatuna budi kuhakikisha kuwa vikwazo vya kibiasha visivyo vya kiforodha (Non-Tariff Barriers) vinashughulikiwa kikamilifu. Utaratibu mahsusi ni lazima uwekwe na utekelezwe kuondoa hivi vikwazo na kama EALA tutatoa wito kwa Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (Summit) kuharakisha mchakato huu. Changamoto nyingine ni pamoja na kusuasua kwenye utekelezaji wa ajenda ya EAC kwenye sera za taifa za nchi wanachama wa Jumuiya. Tutaendelea kushirikiana na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na washikadau wengine kutimiza wajibu wetu kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba ili kuhakikisha kuwa Jumuiya yetu ya kiuchumi inatengemaa.
Ni muhimu kuzingatia kuwa sheria ambazo zinapitishwa na EALA kwa niaba ya EAC zina nguvu ya kisheria na zinatakiwa kupewa kipaumbele kuliko sheria nyingine zilizopo kwenye nchi wanachana kuhusiana na masuala ya Jumuiya. Hivyo basi, tunatoa wito kwa nchi zote wanachama kuharakisha mchakato wa kuhakikisha kuwa sheria za nchi zao zinaoanishwa ili ziweze kuendana na sheria za Jumuiya.
Napenda kutoa wito kwa vyombo vya habari vyote kuwa vishirikiane na EALA katika kutangaza vikao vya Bunge letu katika kipindi hiki cha wiki mbili ambapo tutakuwa tunakutana Dar es Salaam. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment