Friday, August 8, 2014

SI RAYON SPORTS SI AZAM FC


Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,

Imechapishwa Agosti 8, 2014, saa 4:00 usiku

Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara timu ya kandanda ya Azam FC imeanza michuano ya Kagame Cup kwa suluhu ya kutofungana dhidi ya moja ya timu tatu wenyeji wa michuano ya 40 ya Kagame Cup, timu ya Rayon Sports . Mchezo huo wa kundi la kwanza ndio pekee ambao hakutoa goli/magali kati ya michezo mitatu ya kwanza siku ya ufunguzi katika uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.
Mchezo wa kwanza  wa kundi A ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 kati ya KMKM ya Zanzibar na Atlabara ya Sudan Kusini. Mchezo wa pili ulikuwa ni ule kati ya KCCA ya Uganda iliyoichapa Gor Mahia ya Kenya kwa mabao 2-1.
Mchezo wa Rayon na Azam ulikuwa na kasi, huku timu hizo zikicheza kwa mpangilio kuanzia idara ya ulinzi hadi ya kiungo huku safu zote za ushambuliaji  zikikosa umakini licha ya nafasi nyingi kutengenezwa. Ulikuwa ni mchezo wa kusisimua ambao wachezaji wa pande zote walicheza kwa nguvu na kutimiza maagizo muhimu ya walimu wao.
Mambo haya matatu nimeyaona kwa upande wa Azam FC na kwa kiasi kikubwa yamechangia matokeo hayo ambayo yanawafanya kuwa na pointi moja moja kwa kila timu katika kundi A.
SALUM ABUBAKARY ALIPOTEZA NAFASI BORA ZAIDI
Salum Abubakary ni mchezesha timu mzuri. Aliweza kutawala muda mwingi wa mchezo dhidi ya Rayon Sports lakini mchezaji huyo wa kiungo alipoteza nafasi ya wazi pale alipo ' place' pembeni ya lango na kuinyima timu yake bao katika dakika ya 48. Mshambulizi, Kipre Tcheche alikimbia na mpira pembeni ya uwanja upande wa kushoto na kuingia nao katika eneo la hatari na kupiga pasi nzuri ya mwisho kwa Salum ambaye alitokea katikati ya uwanja. Ndani ya hatua sita kiungo huyo alipiga pasi pembeni ya nyavu badala ya kupiga mpira golini akiwa hatua umbali wa hatua zisizozidi sita.

 Nini alichotakiwa kufanya Salum?. Alitakiwa kujibadilisha kutoka sifa za kiungo na kuwa mfungaji. Licha ya hivyo alipoteza umakini na kupiga mpira akiwa amejiamini baada ya kuwa ' huru'. Alifanya kazi nzuri katikati ya uwanja kwa kugawa pasi lakini kitendo cha kupoteza nafasi ya wazi kimechangia matokeo ya sare kwa timu yake.

MBINU ZA KUSAKA MABAO, UMAKINI MDOGO KATIKA UFUNGAJI
Kipre Tcheche alichezewa faulo karibu na maeneo ya hatari na mlinzi wa Rayon Sports katika dakika ya 57. Akapoteza nafasi ya wazi katika dakika ya 64 akiwa karibu na lango akaunganisha bila uelekeo mzuri mpira wa krosi uliotoka wingi ya kulia na kuinyima timu yake nafasi ya kupata bao la kuongoza katika mchezo huo uliokuwa mgumu na mkali muda wote. Safu ya ushambuliaji ya Azam FC ilishindwa kujiamini na kufanya timu yao kupata sare ya bila kufungana.
Didier Kavumbagu aliingia mahali kwa Hamis Mcha ‘ Vialli’ katika dakika ya 70, na kufanya safu ya mashambulizi kuwa na washambuliaji watatu. Kipre, nahodha, John Bocco na Kavu. Azam ilitengeneza nafasi za kutosha katika mchezo huo, na Kavumbagu alitengeneza nafasi nzuri kwa Bocco katika dakika ya 80 lakini mshambulizi huyo wa timu ya Taifa Stars, alipiga mpira huo juu akiwa hatua chache karibu na goli. Hizi ni baadhi tu ya nafasi ambazo Azam walizipoteza na kuonyesha tatizo la umakini wakiwa katika eneo la hatari la timu pinzani.
KUHIMILI MASHAMBULIZI
Mwadini Ally alionekana kufanya makosa katika kipindi cha kwanza baada ya kutema mipira mingi, lakini alipojenga hali ya kujiamini alikuwa mchezaji wa aina yake katika mchezo huo.  Alimnyima bao mshambulizi hatari wa Rayon Sports, Yossa Betram katika dakika ya 75 wakati mshambuliaji huyo alipojaribu kufunga kwa mpira wa kichwa cha kushtukiza akiunganisha mpira wa krosi kutoka upande wa kushoto wa Azam FC
Walinzi, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris na David Mwantika walicheza soka la kazi muda wote japo walitumia robo saa ya mwisho ya mchezo huo kupokea mashambulizi kutoka kwa wenyeji ambao  walipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo. Azam walicheza kwa uvumilivu japokuwa walionekana kuchoka kutokana na kucheza muda mwingi kwa lengo la kupata bao ambalo lilikuwa karibu kupatikana. Matokeo ya sare si haki kwa upande wao kwa sababu walitengeneza nafasi nyingi lakini hazikutumiwa vizuri, lakini matokeo hayo kwa upande mwingine yana afadhali kwa sababu waliyasotea kuyapata.

0714 08 43 08
Chanzo:shaffihdauda.com

No comments:

Post a Comment