Wednesday, August 6, 2014

KURUNZI YA SIMBA SC YAENDELEA KUNASA VIFAA KUSAKA MOTO WA LIGI KUU BARA

 

Aliyekuwa beki wa zamani wa Coastal Union, Abdi Banda (kushoto) amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba sc

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

Imechapishwa Agosti 6, 2014, saa 4:00 asubuhi

WEKUNDU wa Msimbazi wamefanikiwa kumsajili beki wa kushoto wa Coastal Union Abdi Banda baada ya kumuweka kwenye rada zake kwa muda mrefu.
Nyota huyo kinda mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za ulinzi, lakini beki ya kushoto ndio mahala pake haswaa , alisaini mkataba wa miaka mitatu jana na mara moja atajiunga na kikosi cha Simba kinachofanya mazoezi chini ya kocha mkuu, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Banda aliwahi kuripotiwa kuwindwa na Yanga katika dirisha dogo la usajili mwaka huu, lakini ilishindikana kwasababu alikuwa na mkataba na wagosi wa kaya na viongozi wa klabu hiyo walilalamika kitendo cha wanajangwani kumrubuni kijana huyo.
Banda aliwahi kuhojiwa na mtandao huu baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita na alikiri wazi kuwa anatamani kuichezea Simba ingawa alikuwa njia panda kwasababu Yanga nao walimtangazia dau kubwa.
Banda alijipatia umaarufu kwa aina ya uchezaji wake na mpaka kuitwa kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 20, na kama ataendelea kujitunza katika misingi na nidhamu ya mpira, ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kulisaidia Taifa siku za usoni.
Ikiwa katika harakati zake za kujiimarisha na kurudisha makali yake, Simba tayari imeshawasajili wachezaji kadhaa wa nafasi tofauti.
Tayari imewasainisha makipa wawili, kinda Peter Manyika na kipa bora wa ligi kuu msimu uliopita, Hussein Sharrif ‘Iker Casillas’ kutokea kwa wakata miwa wa Mtibwa Sugar.
Pia imeshanasa mabeki Jerome Mvengere, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Siku za karibuni, klabu hiyo pia iliwasajili kiungo mshambuliaji aliyekuwa anaichezea Mtibwa Sugar msimu uliopita, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na mshambuliaji kutoka Ruvu Shooting, Elias Maguri.
Kwasasa Simba inakamilisha taraibu za kuwasajili wachezaji wawili wa kimataifa,  Mkenya Paul Kiongera na Mrundi Pierre Kwizera na tayari wachezaji hao walishagusa ardhi ya bongo na kilichobakia ni kumalizana nao vipengele binafsi.
Kama itafanikiwa kuwasainisha wachezaji hao, Simba itakuwa imekamilisha nafasi tano za wachezaji wa kigeni kwasababu tayari inao watatu ambao ni mabeki Mganda George Owino ‘Gella’ na Mkenye Donald Mosoto pamoja na mfungaji bora wa ligi kuu msimu uliopita, Mrundi, Amiss Tambwe.
Hata hivyo, kamati ya usajili bado inahaha kuangaza kurunzi yake huku na kule ili kuongeza wachezaji wazawa ambapo siku za nyuma, ilielezwa kuwa kocha mkuu, Logarusic alipendekeza asajiliwe, Antony Matogolo na Deus Kaseke kutoka Mbeya City fc.
Pia siku za karibuni kulikuwa na taarifa za usajili wa utata wa mshambuliaji wa Mbeya City fc, Saady Kipanga, ingawa mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka klabuni.

Lakini kipanga ni mchezaji wa Mbeya City na amebakiza mwaka mmoja na nusu, hivyo hakuna bishara ambayo ingefanyika bila kuwahusisha wagonga nyundo hao wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment