Saturday, August 30, 2014

Kivumbi Miss Lake Zone kutimka CCM Kirumba leo

 



Kivumbi Miss Lake Zone kutimka CCM Kirumba leoSHINDANO la Miss Lake Zone 2014, leo linakwenda kufikia tamati katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa kwa warembo 18 kujimwaga jukwaani kuwania taji la kinyang’anyiro hicho kilichovuta hisia za wengi.

Warembo hao waliokuwa wamepiga kambi ya siku 10 katika Lenny Hotel ya Mkoani Geita, leo watachuana kuwania taji linaloshikiliwa na Ruth Charles.

Kwa mujibu wa mratibu wa shindano hilo, Flora Lauwo, warembo wote wapi vizuri wakiwa wamepikwa vizuri na kilichobaki ni muda tu.

“Nashukuru kila mrembo amejifunza na kuona mengi kwa kipindi chote cha kambi, hivyo ni jukumu lake kufanyia kazi yote alitojifunza,” alisema Flora.

Kuhusu ushindani, alisema ni maratajio yake kuwa utakuwa mkubwa kutokana na uwezo wa kila mshiriki ambaye atakuwa akitaka kubeba taji kutwaa zawadi ya gari yenye thamani y ash mil 10.
Alikiri kuwa zwadi hiyo iliyotolewa na mmoja wa wadhamini wa shindano hilo, Lenny Hotel chini ya Mkurugenzi wake Leonard Bugomola ambaye leo ni mgeni rasmi, imeongeza ushindani.

Warembo watakaopanda jukwaani na mikoa yao kwenye mabano ni Moshy Shaban; Doreen Robert; Christina Jilulu (Mwanza); Nikole Sarakikya, Mary Emanuel na Rachael Julika (Shinyanga).
Wengine ni Faudhia Haruna, Jackline Kimambo na Christina John (Kagera), huku Nyangi Warioba; Cecilia Kibada na Everlyn Charles (Simiyu). Wamo pia Martina John; Elinaja Nnko, Winfrida Nashon (Mara)huku Rose Msuya, Rachael Clavery na Faridha Ramadhani wakiwakilisha mkoa wa Geita.

Wakiwa kambini wilayani Geita, warembo hao walifanya shughuli za kijamii ikiwemo kutoa msaada kituo cha Yatima cha Moyo wa Huruma na kutembelea mgodi wa GGM na Hospitali ya Geita na Hifadhi ya Lubondo na kufanya usafi.

Kwa upande wa zawadi, Flora alisema mshindi wa kwanza atazawadiwa gari ya shilingi mil 10; mshindi wa pili ataondoka na bajaji yenye thamani ya sh. mil 4 huku mshindi wa tatu atapata pikipiki y ash mil 1.8.

Mratibu huyo ametoa pongezi kwa wadhamini wakuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji cha Redd’s, Lenny Hotel, Crown Paint, Shule ya Rishor Pre & Primary English Medium na Benki ya CRDB ya Geita.

Flora ambaye ni mara ya tatu kuandaa shindano hilo la Kanda ya Ziwa, amewahi kutoa mara mbili mshindi wa Miss Tanzania (2008 na 2009), Nasrim Karim na Miriam Gerrard. Kwa upande wa kiingilio, Flora alisema viti maalum ni shilingi 30,000; viti vya jukwaa kuu ni sh 10,000 na viti vya kawaida ni sh 5,000.

No comments:

Post a Comment