Thursday, September 4, 2014

BILIONI 1.3 ZATUMIKA KUJENGA MAABARA ZA SAYANSI NA HOSTELI


IMG_20140903_160958
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Pudenciana Kisaka akizungumza
Na Denis Mlowe,Iringa
JUMLA ya sh. bilioni 1.3 zimetumika katika ujenzi wa maabara za sayansi, hosteli za wasichana na chumba cha darasa katika shule za sekondari za Ismani, Nyang’ro na Kalenga zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
 
Akizungumza na wahabari hivi karibuni ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Iringa,Pudenciana Kisaka  alisema kuwa halmashauri kupitia idara ya elimu Sekondari imekamilisha maabara tatu za masomo ya sayansi , chumba cha darasa na hostel katika shule hizo zilizokuwa zina upungufu wa majengo hayo.
 
Alisema kuwa maabara moja imejengwa katika shule ya sekondari Ismani na ujenzi wake kukamilika  kwa asilimia 100 na inatumika kwa masomo ya Bailojia na imegharimu zaidi ya shilingi milioni 89.
 
Kisaka alisema shule ya sekondari Kalenga imejengewa maabara mbili ambazo zimekamilika kujengwa na zinatumika kwa masomo ya Fizikia na Kemia na kugharimu shilingi milioni 29.
 
Aidha alisema halmashauri hiyo imejenga hostel ya wasichana wa shule ya sekondari Kalenga ambao umegharimu sh. Milioni 258 mpaka kukamilika na ujenzi wa chumba kimoja cha darasa shule ya sekondari Nyang’oro  uliogharimu sh. Milioni 13.
Kisaka akizungumzia kuhusu mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano alisema idara ya elimu imepangiwa jumla ya wanafunzi 2389 wa kidato cha tano katika shule sita hivyo idadi imeongezeka kutoka 1433 mpaka 2389 sawa na asilimi 156 ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopokelewa kwa mwaka 2013/2014 walikuwa 1433 sawa na asilimia 93.

No comments:

Post a Comment