Friday, September 26, 2014

SIMBA, YANGA SASA KUMALIZANA OKTOBA 18...NI JAJA AU OKWI?


MECHI ya Simba na Yanga iliyopangwa kuchezwa Oktoba 12 kwenye Uwanja wa Taifa sasa imesogezwa mbele mpaka Oktoba 18 kupisha mechi ya kirafiki ya Taifa Stars na Benin.Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza jana kwamba Stars itacheza Oktoba 12 na leo watatangaza mabadiliko mapya ya ratiba ya Ligi kupisha mechi hiyo ya kalenda ya Fifa na ni rasmi kwamba Simba na Yanga ni wikiendi ya Oktoba 18.
Benin itakuja nchini Oktoba 10 na msafara wa watu 28. Pambano la Stars na Benin litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Wakati huo huo, kutokana na mechi hiyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom inafanyiwa marekebisho madogo, na marekebisho hayo yatatangazwa leo Ijumaa siku ambayo pia Rais wa TFF, Jamal Malinzi atafunga mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa vyama vya mpira wa miguu wa wanawake vya mikoa ya Tanzania Bara kwenye ofisi za TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ya siku tano yalishirikisha viongozi 34 wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari na Meneja wa Twiga Stars, na yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry Tandau.
Chanzo: Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment