Saturday, September 6, 2014

PATRICK PHIRI LAZIMA AIFUNGE GOR MAHIA LEO?

 
Mshambuliaji wa Simba sc, Mkenya Raphael Kiongera (kushoto) akimtoka beki wa Zesco United, Benard Mapili katika mechi ya Tamasha la Simba Day, Agosti 9 mwaka huu. Msimbazi walilala 3-0 uwanja wa Taifa.

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KARIBIA mwezi mmoja sasa tangu klabu ya Simba imfungashie virago aliyekuwa kocha mkuu, Mcroatia Zdravko Logarusic.
Tukio hilo lilijiri muda mfupi baada ya Simba kubamizwa mabao 3-0  katika mechi maalumu ya Tamasha la Simba ‘Simba Day’ (Agosti 9 mwaka huu) iliyopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Zesco United ya Zambia.
Loga katika mechi hiyo alifanya mabadiliko ya wachezaji takribani 8 kwa lengo la kuwajaribu, wakiwemo wale waliokuja kufanya majaribio kutoka Botswana, Kenya na Gambia.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuinusuruu Simba na kipigo hicho kilichozua mengi hasa baada ya  Loga kuwatamkia maneno mabaya baadhi ya wachezaji wakongwe kama vile Amri Kiemba na Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Loga aliyekuwa ametoka kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa Simba alivunjiwa mkataba huo na uongozi wa Simba na hatimaye kuajiriwa kwa Mzambia Patrick Phiri.
Kurudi kwa Phiri kulileta faraja kubwa kwa wachezaji wengi wa Simba waliokuwa wanampinga Loga kutokana na ukali uliozidi kipimo.
Phiri ni kocha anayeifahamu Simba vizuri kwasababu hii ni mara ya tatu kuiongoza, na ana rekodi ya kuipa ubingwa bila kufungwa mwaka 2009.
Ujio wa Mzambia huyo umerudisha morali kwa wachezaji wa Simba waliokuwepo kikosini kabla ya dirisha la usajili na wale waliosajiliwa majira ya kiangazi.
Amiss Tambwe (kulia) hatacheza leo

Kwa bahati nzuri kocha huyo anaonekana kupendwa na wapenzi wengi wa Simba wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu kwasababu historia inamlinda kwa kiasi kikubwa.
Phiri aliweka kambi kisiwani Unguja na huko ndiko alitumia muda mwingi kuandaa kikosi chake kwa ajili ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Akiwa huko kocha huyu atakayekuwa mpinzani namba moja kwa Marcio Maximo wa Yanga amekuwa akifanyia kazi mambo matatu makubwa katika kikosi cha Simba.
Moja; amekuwa akiwafundisha wachezaji wake namna ya kumiliki mpira kwa asilimia kubwa uwanjani. Lengo la Phiri ni kuifanya Simba icheze zaidi uwanjani ikiwa na mpira ili kuwafanya wapinzani wachanganyikiwe.
Kumiliki mpira kwa kiwango cha juu husaidia zaidi kuwapa presha wachezaji pinzani na kufungua mlango wa kupanga mashambulizi.
Pili; kocha huyu amekuwa akihangaika kuwafundisha wachezaji wake namna ya upigaji wa pasi sahihi. Lengo ni kufuta pasi zisizokuwa na macho kwa wachezaji wa Simba, Utamaduni wa Simba unaofahamika kwa muda mrefu ni kupiga pasi fupifupi na haraka.
Phiri analifahamu hilo na ndio maana anawajenga wachezaji wake katika msingi huo.
Tatu; Phiri amekuwa akihangaika kuwafundisha wachezaji wake namna ya kupanga mashambulizi ya kasi. Kwa muda mrefu amekuwa akihangaika na safu ya ushambuliaji na kiungo ili ziwe na ushirikiano mzuri wa kupanga mashambulizi ya uhakika.
Rais wa Simba sc, Evans Aveva (wa kwanza kushoto) alishuhudia Simba ikichapwa 3-0 na Zesco Tamasha la Simba Day. Kulia ni aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic

Pia Phiri amefanya kazi ya kuwaweka pamoja wachezaji baada ya presha ya Loga. Lengo ni kurudisha morali kwa wanandinga hao.
Kama ulibahatika kuiangalia Simba ikicheza Zanzibar akicheza mechi za kirafiki au mazoezi ya Simba kuna kitu kipya kimeongezeka.
Wachezaji wanaonekana kuonana na kucheza kitimu zaidi. Hii ni kwasababu ya kocha Phiri ambaye amewaweka pamoja tena.
Leo hii Simba sc inacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Hii ni mechi ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki kwa Patrick Phiri tangu arejea Msimbazi. Kitakuwa kipimo kizuri kwake.
Pia mashabiki wa Simba wanaoishi Dar es salaam wataiona timu yao ikicheza uwanja wa Taifa chini ya Phiri, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya wachezaji muhimu watakosekana katika kikosi  hicho kutokana na majukumu ya timu ya Taifa.
Joram Mgeveke, Haroun Chanongo, Ramadhan Singano ‘Messi’, Amri Kiemba, hawataonekana leo kwasababu wapo na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi kesho mjini Bujumbura.
Pia Amis Tambwe, Piere Kwizera wapo na timu ya taifa ya Burundi, hivyo watakosekana.
Kocha mkuu wa Simba sc, Patrick Phiri

Hata hivyo wachezaji kama Masoud Cholo, Miraji Adam, Hussein Sharrif, Ivo Mapunda, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Uhuru Seleman, Shaaban Kisiga, Said Ndemla, Abdallah Seseme, Abdi Banda, Emmanuel Okwi na wengine ambao sijawataja wataweza kuiwakilisha Simba.
Kimpira, kikosi cha Phiri kitaathirika kwa kiwango fulani kwa kukosa wachezaji muhimu, lakini sio sababu ya kufanya vibaya.
Simba ina wachezaji wengi wanaofanya mazoezi na kwa muda aliokaa Simba tangu aanze kazi, Phiri anajua ni nani anaweza kucheza kikosi cha kwanza na mbadala wake ni nani.
Katika mechi za kirafiki Zanzibar, Phiri alikuwa anachezesha vikosi viwili kwa lengo la kupata timu ya kwanza na wachezaji mbadala wa kikosi cha kwanza.
Kwa kuwa bado hajaamua timu ya kwanza ni ipi, kila mchezaji anajituma kutafuta nafasi ya kuonwa. Kwa mazingira hayo kila anayepangwa anapigana kumshawishi Phiri.
Leo hii naitegemea Simba mpya inayocheza pasi za uhakika, kasi ya kutosha, umiliki wa mpira na mashambulizi ya nguvu. Nasema hivi kwasababu Phiri amekuwa akiifundisha timu yake katika aina ya mpira wa hivi.
Lakini siwapi Simba asilimia zote za kushinda mechi ya leo kutokana na aina ya mpinzani wake, ila inaweza kushinda.
Gor Mahia imekaa pamoja kwa muda mrefu na ilishiriki michuano ya kombe la Kagame iliyomalizika mwezi uliopita mjini Kigali, Rwanda.
Phiri akiwa kazini

Japokuwa ilitolewa hatua ya makundi, lakini ilionesha kiwango cha juu na ina wachezaji wazuri wanaoweza kuipa changamoto nzuri Simba.
Kutokana na ubora wa Gor Mahia, nadhani hesabu za Phiri zinatakiwa kukaa sawa zaidi ili kuipa ushindi timu yake.
Hii ni mechi ya kirafiki tu, lakini ina maana kubwa kwa Phiri ili kuwaaminisha mashabiki wa klabu hiyo, ikizingatiwa upande wa pili wamekuwa wakifanya vizuri na katikati ya wiki waliifunga Thika United bao 1-0 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Cha msingi ni kwamba, mashabiki wa Simba lazima watambue kuwa Gor Mahia ni wazuri na si rahisi kuwafunga.
Kama itatokea timu ikacheza tofauti na matarajio yao, watakiwa kuwa na uvumilivu kwasababu ndio kwanza timu inaandaliwa.
Katika mechi za majaribio, makocha wanaangalia vitu vingi. Wachezaji wanajaribiwa kwa nafasi tofauti.Kama ukiona Fulani kapangwa namba tofauti, ujue kuna kitu kocha anakitafuta.
Wanasimba wasiende uwanjani kwa tambo na kuwaangali Yanga wamefanya nini. Phiri na Maximo ni makocha wawili tofauti na aina ya wachezaji wao ni tofauti.
Kama Yanga imeifunga Thika United ya Kenya, sio lazima Simba kuifunga Gor Mahia ya Kenya. Ni timu mbili tofauti.
Phiri ni kocha mzuri na rekodi yake haina wasiwasi kwa Simba, lakini kwa muda huu bado yuko kipindi cha mpito akitafuta timu ya ushindani.
Anaweza kuwatumia wachezaji wengi leo hii kwasababu ni mechi nzuri ya kimataifa ya kirafiki. Lengo lake ni kuona namna wanasoka wake walivyomuelewe.
Nina imani kubwa na Phiri. Ni aina ya makocha ninaodhani wanaweza kulisaidia soka la Tanzania, lakini naamini Wanasimba watampa muda Mzambia huyu.
Rekodi ya nyuma isiwafanye wavimbe vichwa, mpira umebadilika na kutoka 2009 akichukua ubingwa bila kufungwa mpaka sasa kuna mambo mengi yametokea katika mpira wa Tanzania.
Kuna Azam fc, Mbeya City FC, Kagera Sugar, Ruvu Shooting na timu nyinginezo. Upinzani umekuwa mkubwa, hivyo Phiri lazima atahitaji kushindana zaidi.
Kwa mazingira ya sasa, Phiri sio lazima aweke rekodi kama za nyuma na ndio maana hata Jose Mourinho aliyetamba na Chelsea miaka ya 2006, aliporudi msimu uliopita alimaliza bila kikombe.
Sitegemei kuona mashabiki wanaizomea timu kwa namna yoyote ile, kocha anahitaji muda pamoja na wachezaji wake.
Vijana wamekuwa wakifanya mazoezi magumu na mepesi, hata miila yao bado haijawa tayari sana kwa kutandaza soka. Tusitegemee makubwa kutoka kwao katika mchezo wa leo.

Kila la kheri Simba sc katika mchezo wa leo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

No comments:

Post a Comment