Tuesday, September 2, 2014

Serikali yabaini kilogram 6,428.12 za dawa za kulevya mwaka 2013

       
Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bi.Gloria Omari akiongea na waandishi wa Habari( Hawapo pichani) kuhusu Hali ya Dawa za Kulevya kwa Mwaka 2013 nchini ambapo amesema jumla ya majalada 208 yalipokelewa na kufanyiwa uchunguzi, wakati wa mkutano leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa.
Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Kemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bw. Elias Mulima akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu matumizi ya dawa aina ya Cocaine hospitalini kama tiba hasa kwa wagonjwa wenye maumivu makali na wanaofanyiwa upasuaji, wakati wa Mkutano uliofanyika Leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Ofisi hiyo Bi.Gloria Omari.
(Picha na Hassan Silayo -MAELEZO)
……………………………………………
Na Fatma Salum MAELEZO
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imefanikiwa kubaini jumla ya kilogram 6,428.12 za sampuli mbalimbali za dawa za kulevya kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2013.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Bi.Gloria Omari katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Bi Gloria alisema kuwa kiasi hicho cha madawa kimepatikana baada ya uchunguzi wa majalada 208 yaliyopokelewa na kufanyiwa uchunguzi katika mwaka huo.
“Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umefanya Uchunguzi wa vielelezo vidhaniwavyo kuwa ni dawa za kulevya ambapo majalada 208 yaliyopokelewa kwa mwaka 2013 na kubaini jumla ya kilogram 6,428.12 za dawa hizo”Alsema Bi. Gloria.
Akitaja idadi ya majalada na sampuli za dawa hizo Bi Gloria alisema kuwa dawa aina ya Bangi imeongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha uzito wa sampuli ikiwa na kilogram 3765.12 kwa idadi ya majalada 72 wakati Heroin imeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya majalada ambapo majalada 112 yalichunguzwa na kilogram 46.67 ziligunduliwa.
Aina nyingine ya dawa zilizotajwa ni Cocaine ikiwa na idadi ya majalada mawili yaliyochunguzwa na kilogram 4.22 ziligunduliwa, majalada 21 ya mirungi yalichunguzwa na kupatikana kilogram 2579.8 na jalada moja la Ephedrine lilikuwa na kilogram 32.31.
Bi Gloria aliongeza kuwa shughuli za uchunguzi wa sampuli za dawa hizo umesaidia utoaji wa ushahidi mahakamani pamoja na kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Akijibu swali la waandishi wa habari  Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Kemia kutoka Ofisi hiyo  Bw. Elias Mulima alibainisha kuwa  kuna uhalali wa matumizi ya dawa aina ya Cocaine hospitalini kama tiba hasa kwa wagonjwa wenye maumivu makali na wanaofanyiwa upasuaji.

No comments:

Post a Comment