Tuesday, September 23, 2014

MANISPAA YA ILALA YAJIPANGA KUWA NA BARABARA ZENYE HALI BORA

    Afisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bi Tabu Shaibu akiwaeleza waandishi wa Habari (Hawapo pichani) waandishi wa Habari kuhusu Miradi iliyotekelezwa kwa ajili ya kupunguza msongamano katika halmashauri hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bw. Frank Mvungi.
 

     Mhandisi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bw. Batimagwa James akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu hatua zinazochukuliwa na Manispaa hiyo katika kuhakikisha barabara zinakuwa kwenye hali nzuri katika kipindi chote cha mwaka.kulia ni Afisa Uhusiano wa Halmashauri hiyo Bi Tabu Shaibu
 
HASSAN SILAYO-MAELEZO

 
 
 
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Idara ya Ujenzi inahudumia barabara zenye urefu wa kilomita 536.9 ambazo kati ya hizo kilomita 144.2 ni za lami, kilomita 64.7 ni za Changarawe na kilomita 328 ni za udongo.  Huduma hizi ni pamoja na kujenga, kukarabati na kusimamia sheria za matumizi ya barabara katika eneo la Manispaa ya Ilala.
MIRADI ILIYOTEKELEZWA HADI SASA KWA AJILI YA KUPUNGUZA NSONGAMANO
Ujenzi wa Barabara ya Mazengo hadi Kibasila kwa kiwango cha Lami Km.1.2
Ujenzi wa Barabara ya Lindi kwa kiwango cha Lami Km. 0.7
Ujenzi wa barabara ya Vingunguti  Baracuda- urefu wa 1.3 km unaendelea na tayari mita 880 ziko hatua kuanza kuweka lami nyepesi na lami ngumu. 
UCHONGAJI WA BARABARA ZA UDONGO
Halmashauri imeweza kutekeleza kazi za uchongaji wa barabara za udongo na changarawe kwa kutumia greda lake moja.  Barabara zilizochongwa ni za maeneo ya kata za Ukonga, Pugu, Majohe, Kivule, Msongola, Chanika, Kitunda, Kinyerezi, Tabata, Kimanga, Gongolamboto, Kipawa, Kiwalani, Vingunguti, Upanga Mashariki, upanga Magharibi, Gerezani Ilala, Jangwani, Mchikichini na Buguruni. Barabara hizi zimekuwa zikiharibika wakati wa kipindi cha mvua zinapokuwa nyingi mathalani mvua zilizonyesha katika Mkoa wa Dares Salaam na kuleta maafa. Barabara nyingi ziliharibika kiasi cha kutopitika kabisa hali iliyoathiri huduma mbalimbali.
Kwa kuliona hilo na kuhakikisha kuwa Barabara hizi zinapitika wakati wote Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imenunua Magreda mawili (2) kwa gharama ya Tshs 1.2 billioni. Pamoja na jitihada hizo yapo maeneo mawili ambayo kwa sasa ni kero
ENEO LA HYDARI PLAZA
Eneo hili hujaa maji wakati wa Mvua kutokana na kuwepo kwa Chemba za Maji taka zinazotiririsha maji barabarani na kusababisha mashimo ambayo yamekuwa adha kwa watumiaji wa barabara hiyo. Halmashauri imekuwa ikiziba viraka vya lami bila mafaikio. DAWASCO ambao ndiyo wamiliki wa chemba hizo wametakiwa kuzikarabati chemba zao.  Halmashauri inaendelea na maandalizi ya kuweka zege badala ya lami ili eneo hilo liweze kupitika kwa urahisi.  Kazi hii itafanyika mapema katika mwaka huu wa fedha 2014/2015.
ENEO LA SHULE YA UHURU WASICHANA HADI UHURU MCHANGANYIKO – BARABARA YA LINDI
Eneo hili lilifanyiwa ukarabati wa mfereji wa maji ya mvua ili kuyaingiza katika kalavati kuu lilopo katikati ya barabara ya Mismbazi, kisha lami iliwekwa.  Lakini kufuatia eneo hilo kutumiwa na Daladala za Temeke/Tandika – Kariakoo bila udhibiti wa kutosha wameharibu mferefi huo na kusababisha maji kutuama na kuharibu tabaka lote la lami,  Halmashauri ina kusudia kuujenga upya mfumo wa maji ya mvua na kuweka lami kipande hicho katika mwaka wa fedha 2014/2015.
 
MASHIMO YA BARABARANI
Uchakavu wa barabara za lami hasa maeneo ya katikati ya Jiji (Kata na Gerezani, Kivukoni, Kisutu, Mchafukoge, Jangwani, Kariakoo, Upanga mashariki na magharibi). Hali hii inatokana na barabara nyingi katika maeneo haya kuchoka (kuzeeka) kwani nyingi zilijengwa katika miaka ya 1990. Uchakavu huu unachangia kuwepo kwa mashimo mengi kwakuwa zinaharibika kwa wakati mmoja.
Jambo lingine linalochangia uharibifu wa barabara na kuwa na mashimo ni ukataji ovyo wa barabara kwa lengo la kuweka na kukarabati miundombinu ya maji safi na taka na mikonga ya mawasiliano ya simu. Wakandarasi ambao hurusiwa kufanya kazi hiyo huchukua muda mrefu kurejesha barabara katika hali ya awali. Hali inasababisha maji ya mvua kutuama na kuharibu tabaka la barabara. Halmashauri imekuwa ikiyaziba mashimo hayo kulingana na hali ya upatijanaji wa fedha, Hata hivyo bado hali haijawa bora kwani Barabara hizi zinahitaji matengenezo makubwa ya kuwekwa Lami upya.
 
CHANGAMOTO
·         Uhaba wa fedha za kukidhi mahitaji ya matengenezo mapya na ukarabati wa barabara, madaraja makalavati na mifereji ya maji ya mvua ukilinganisha na ukubwa wa mtandao wa barabara.
·         Ukataji holela wa barabara kwa malengo ya kuweka mifumo ya maji safi, maji taka, mawasiliano (fibre cables), n.k kinyume cha utaratibu ambapo Halmashauri hutoa vibali na kusimamia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibiwa.
·         Wizi wa mifuniko ya chemba za maji ya mvua kwa ajili ya biashara ya chuma chakavu. 
·         Utupaji ovyo wa taka na michanga barabarani, hali hii inasababisha kuziba kwa mifereji ya maji ya mvua na kusababisha uharibu wa barabara kutokana na mafuriko, madibwi makubwa ya maji.  Hii ni kero kwa watumiaji wa barabara.
·         Wananchi kuunganisha mfumo wa maji taka ya majumbani kwenda mifereji ya maji ya Mvua.  Hususan katika Kata za Gerezani, Kariakoo, Jangwani, Kisutu na Mchafukoge ambapo baadhi yao wamekamatwa na kutozwa faini na kisha kuziba mifumo hiyo.  Kitendo hiki kinasababisha kuwepo kwa harufu mbaya katika maeneo mbalimbali kwa watumiaji wa Barabara. 
 
Mikakakati
·         Halmashauri inaendele a kuweka mifuniko ya mifereji ya maji ya mvua. Hadi sasa jumla ya mifuniko 410, ambapo 250 imewekwa kwenye chemba zilizo kuwa wazi na 160 ipo kwa ajii ya dharura
·         Kujenga mifereji mipya ya maji ya mvua katika sehemu korofi.
·         Kuunda kitengo kitakachodhibiti uzito wa magari kwa kuweka mizani zinazohamishika katika maingilio yote ya barabara kuu za kuingia katikati ya Halmashauri kwa masaa 24.
 
Imeandaliwa na;
Tabu F.Shaibu- Afisa Uhusiano
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment