Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe leo amezindua magari 54 ya abiria ya Chama cha Ushirika cha Madereva wa Taksi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam yenye thamani ya sh. Milioni 840 kuboresha usafiri wa abiria.
Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika katika eneo la kiwanja cha zamani cha Ndege, Terminal I, makao makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambapo ameiagiza TAA kuhakikisha inaipa hadhi JNIA kama alivyokuwa mwenye jina hilo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“TAA hakikisheni JNIA inabeba jina la Julius Nyerere kwa mandhari, utendaji na vyombo vya usafiri, “ Waziri Mwakyembe amemweleza Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Moses Malaki na uongozi wa TAA kwa jumla.
Waziri Mwakyembe amesema, hatua ya ATACOS kununua magari hayo inaongeza ubora wa huduma na hadhi ya kiwanja cha ndege cha JNIA na kwamba magari hayo yatasaidia kuchukua hata wageni wa Serikali
Alisema mradi huo wa magari ni mkubwa kwa wana ushirika hao na magari yao ni ya viwango vya juu na hata kwa mbali ukiyaangalia magari hayo, yana viwango vikubwa na Serikali ikipata wageni zaidi ya 500 kwa mpigo, haitahangika kutafuta magari kwani hayo yapo. Thamani ya gari moja ni sh. Milioni 15 na ni mkopo wa Equity Bank.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe amewataka madereva hao kuzingatia usafi wa magari na wao wenyewe kwani wageni wakikodi magari hayo na kuyakuta ni nadhifu na wao ni wasafi, ndio kielelezo cha nchi yetu.
“Naheshimu sana kazi mnayofanya. Ina add value (ongeza thamani), “ waziri Mwakyembe amesema na kuutaka uongozi wa TAA utambue mchango wa madereva hao kwani magari yao ni mazuri na hata katika jengo la tatu la abiria (TB III) linalojengwa, yanaweza kupewa fursa.
Amewataka kuyatunza kwa kuyavika vita vyeupe na wao kuvaa sare nyeupe na kusimamia viwango kwa kuwa na zaidi ya sare moja nyeupe ili hata akiingia mtalii, ajue kuwa anaingia nchi ya wastarabu.
Hata hivyo, Waziri Mwakyembe ameeleza kusikitishwa na madereva hao kuushitaki uongozi wa TAA mahakamani kuhusu haki ya kuendesha biashara ya taksi JNIA. Amewaeleza asingeweza kuwasaidia kutatua kero hiyo kwa kuwa kuna kesi hiyo bado iko mahakamani hadi leo.
“Sijui nani aliwashauri. Mimi ni Kiongozi wa Serikali tena ni Wakili wa Mahakama Kuu. Siwezi kuingilia utendaji wa mhimili mwingine wa chombo cha haki. Nitaonekana wa ajabu. Mikono yangu imefungwa katika hili, “ aliwaeleza na kuacha kujibu kero zao kuhusu mgogoro huo.
Katika risala yao kwa Waziri Mwakyembe, Katibu wa stendi ya madereva teksi JNIA, Mohammed Mashombo amemweleza Waziri mafanikio na kero zao tangu waanze 2000 na kuomba awasaidie.
Hata hivyo, uongozi wa TAA ulimweleza Waziri Mwakyembe awali kuwa, madereva hao waliushitaki kuhusiana na mkataba wa kufanya biashara JNIA na kesi hiyo inaendelea hadi leo na kwamba mengi ya madai waliyomtaka awasaidie, ndio wameyewasilisha mahakamani.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wageni mbalimbali na watendaji wa TAA, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Meneja wa TRA Mkoa wa Temeke, Mkurugenzi wa Equity Bank, Mkurugenzi wa ABG na Afisa Biashara wa Manispaa Temeke.
Imetolewa na Godfrey John Lutego
Afisa Uhusiano – Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
No comments:
Post a Comment