Friday, September 26, 2014

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekamilisha mradi wa kuboresha kituo cha kupokea na kutuma mawasiliano

Afisa Habari wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Bestina Magutu akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kukamilika kwa maboresho ya kituo cha Mawasiliano ya Radio kwa ajili ya usafiri wa anga kilichopo Mnyusi mkoani Tanga, kilichojengwa na kampuni ya JATRON ya Norway, wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mhandisi Mkuu toka Mamlaka Hiyo Bi. Valentine Kayombo.

Mhandishi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Valentine Kayombo akiwaeleza waandishi wa Habari(Hawapo pichani) faida zitakazopatikana kutokana na kukamilika kwa Kituo hicho ikiwamo kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za uongozaji ndege, wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Mamlaka Hiyo Bi. Bestina Magutu.

 Inspeka Mwandamizi Idara ya Udhibiti Usalama wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Redemptus Bugumula akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu ongezeko la marubani wanawake nchini ambao wanafikia Takribani Kumi kwa sasa wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mhandisi Mkuu toka Mamlaka Hiyo Bi.Valentine Kayombo.

Picha na Hassan Silayo-MAELEZO



Frank Mvungi-Maelezo

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekamilisha mradi wa kuboresha kituo cha kupokea na kutuma mawasiliano ya radio zinazotumika katika usafiri wa anga kilichoko Mnyuzi mkoani Tanga.

Mradi huo  uliojengwa na kampuni ya JOTRON ya NORWAY umegharimu Serikali zaidi ya shilingi milioni 200 na ulikabidhiwa rasmi kwa  TCAA mapema mwezi Agosti mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Habari wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Bestina Magutu wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.

Magutu alisema kuwa  kukamilika kwa kituo hicho kumeongeza ufanisi wa utoaji huduma za uongozaji ndege na kuimarisha zaidi usalama wa safari za anga hapa nchini.

Akifafanua zaidi Magutu amesema hali hiyo itachangia kuongezeka kwa mapato ya Mamlaka hiyo yanayotokana na tozo la huduma za uongozaji ndege.

Akizungumzia mikakati ya Mamlaka hiyo Magutu amesema inaendelea kuwekeza katika miundo mbinu ya kuongozea ndege hivyo kwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia pamoja na kumudu ukuaji wa Sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mamlaka hiyo imesema kuwa wanafunzi watano waliopewa ufadhili  wa kusomea urubani nchini Afrika ya Kusini wameendelea kupata ufaulu wa juu na kushika nafasi ya kwanza hadi ya tano katika darasa la watu 14 katika shule ya urubani nchini Afrika ya Kusini.
Takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha ongezeko la miruko ya ndege ( flight movements) kutoka 222,430 mwaka 2012 hadi kufikia miruko 230,458 sawa na ongezeko la asilimia 3.6 kadhalika katika kipindi hicho idadi ya abiria imeongezeka kutoka 4,056,925 hadi kufikia 4,626,016 sawa na ongezeko la asilimia 14.Idadi ya abiria inatarajiwa kufika zaidi ya milioni 5 kufikia mwishoni mwa mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment