Kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed akiokoa moja ya shambulizi la Yanga. (Picha na Globalpublisher)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
PAZIA la ligi kuu Vodacom Tanzania Bara limepenuliwa jana kwa mechi sita kupigwa viwanja mbalimbali nchini.
Ni mechi zilizoangaliwa na kutazamwa kwa umakini na mashabiki wengi wa soka, lakini mtanange wa Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga uwanja wa Jamhuri ulivuta hisia za mashabiki wengi.
Kwa kuzingatia idadi kubwa ya mashabiki waliofurika uwanjani, ni dhahiri mechi hii ilikuwa na mvuto kwa watu wengi waliotamani kuiona Yanga ya Marcio Maximo ikifanya vitu vyake.
Zaidi Geilson Santos Santana ‘Jaja’ akitokea kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam fc, Ngao ya Jamii, alikuwa kivutio kikubwa.
Matokeo ya mechi za jana yalikuwa kama ifuatavyo kwenye jedwali hilo hapo chini:
TIMU
|
MATOKEO
|
Mtibwa Sugar v Young Africans
|
2-0
|
Stand United v Ndanda fc
|
1-4
|
Mgambo JKT v Kagera Sugar
|
1-0
|
Azam fc v Polisi Morogoro
|
3-1
|
Ruvu Shootings v Tanzania Prisons
|
0-2
|
Mbeya City v JKT Ruvu
|
0-0
|
Ukitazama mechi sita zilizopigwa jana, timu tatu tu zilipata ushindi katika mechi za nyumbani ambazo ni Azam, Mtibwa Sugar na Mgambo JKT.
Timu mbili zilipoteza mechi nyumbani ambazo ni Ruvu Shooting na Stand United, wakati Mbeya City fc pekee ndio walitoka suluhu wakiwa nyumbani.
Tanzania Prisons msimu uliopita walianza msimu kwa kufungwa mechi mbili za kwanza ugenini, lakini msimu huu wameanza na ushindi wa ugenini.
Japokuwa ni mapema, lakini hii inaweza kutoa picha kuwa maafande hao chini ya kocha David Mwamwaja wamejipanga vizuri na ndio maana waliwashinda katika uwanja mgumu wa Mabatini.
Kocha wa timu hiyo, David Mwamwaja wakati akijiandaa na msimu mpya, mara kadhaa alikuwa anasema msimu huu hawataki biashara ya dakika za mwisho bali wanataka kufunga mahesabu mapema.
Kocha huyo alikuwa anamaanisha hawatakubali kupoteza mechi nyingi za mzunguko wa kwanza na wataanza kwa ushindi, hatimaye maneno yake yametimia jana.
Kikosi cha Mbeya City fc kilichoanza jana dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Sokoine Mbeya
Licha ya kushinda, Prisons walionekana kuwa wapya na kuonesha ushindani mkubwa mbele ya kikosi cha Tom Alex Olaba.
Inawezekana timu hii inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania akifanya vizuri kama itaendelea kuwa na nidhamu ya mpira kama walivyofanya jana.
Ndanda fc wameanza kwa ushindi katika mechi yao ya kwanza ya ligi kuu kwa kuitandika 4-1 Stand United ugenini.
Tangu dunia hii kuumbwa na Mwenye Enzi Mungu, hiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa timu hii ya Mkoani Mtwara kucheza ligi kuu na kushinda mabao mengi ugenini.
Mechi hii ilizichonganisha vibaya timu mbili zilizopanda daraja pamoja. Upinzani mkubwa ulitegemewa na makocha wa timu zote waliingia kwa tahadhari kwasababu walijua ni sehemu pekee ya kuanza kwa pointi.
Mzani wa Ndanda fc na Stand United unafanana kwa kiwango kikubwa na ndio maana haikuwa rahisi kujua timu gani ingeshinda.
Watu wa Mtwara wamekuwa wakisisitiza kuisapoti timu yao kwa kuwa na ‘slogan’ maarufu, ‘Ndanda fc kwanza, Simba,Yanga baadaye’.
Jana wameanza kwa ushindi, hakika ni jambo jema kwao, limewaongezea morali na litawafanya wajiamini na kupambana zaidi mechi zijazo.
Ni mapema sana, lakini kwa soka waliloonesha Ndanda fc, unaweza kuwatabiria kufanya vizuri msimu huu.
Nahodha wa Tanzania Prisons (kushoto) na Ruvu Shootings (kulia) wakiwasalimia waamuzi kabla ya kuanza mechi jana Mabatini
Mbeya City kwa ‘staili’ ile ile ya msimu uliopita wameanza kwa suluhu. Kumbukumbu zinaonesha kuwa katika mechi ya kwanza mwaka jana walianza kwa suluhu (0-0) dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Sokoine Mbeya.
Jana wameanza na matokeo kama hayo nyumbani dhidi ya JKT Ruvu. Hii ina maanisha wamerudia rekodi yao, lakini huwezi kutambua kama watafanya hivyo na msimu huu.
Mbeya City ilicheza vizuri, ilitengeneza nafasi kadhaa lakini haikuweza kufunga. Pengine nidhamu kubwa ya JKT Ruvu na kiwango chake kizuri kiliwanyima nafasi ya kushinda mechi hiyo.
City wanatakiwa kujipanga kwasababu ni moja ya timu nne za juu, hivyo timu zinakwenda kucheza nayo kwa tahadhari kubwa.
Kama watapunguza nidhamu ya mchezo, wanaweza kushindwa kurudia rekodi yao ya mwaka jana.
Mgambo nao wameonekana kuja kivingine kama ilivyo kwa Prisons. Msimu uliopita walianza vibaya na walijinusuru kushuka daraja dakika za majeruhi, lakini jana wameonesha uwezo mzuri dhidi ya Kagera Sugar.
Kikosi chao kimebadilika na kina morali kubwa ya uwanjani. Hii ni dalili nzuri kwao na wameoneka kuwa katika nidhamu ya mpira. Haitakuwa rahisi kuchukua pointi tatu uwanja wa Mkwakwani.
Mabao mawili ya Didier Kavumbagu na moja la Aggrey Morris yalitosha kuwapa Azam fc ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro.
Nahoda Bakari aliifungia Polisi Moro bao la kufutia machozi katika mechi yao ya ufunguzi.
Kikosi cha JKT Ruvu kilichoanza jana dhidi ya Mbeya City fc uwanja wa Sokoine
Azam fc ambao ndio mabingwa watetezi walicheza vizuri katika mechi ya jana na kuwazidi Polisi vitu vingi.
Kiufundi, Azam fc walikuwa na mipango sahihi kuliko Polisi Moro walioonekana kuwa na mchecheto hususani kipindi cha kwanza.
Pengine ugeni ulichangia, lakini ulikuwa mtihani mkubwa kwao kwasababu Azam ni timu bora na imekaa pamoja kwa muda mrefu.
Licha ya kutoka kufungwa mabao 3-0 na Yanga katika mechi ya Ngao ya jamii, jumapili iliyopita, Azam fc walionekana kuwa na mabadiliko makubwa ya uchezaji.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog aliwaanzisha wachezaji kadhaa ambao hawakucheza mechi ya Ngao ya jamii.
Kipa Aishi Manula alianza badala ya Mwadini Ali, Kinda Gadiel Michael naye alianza badala ya Erasto Nyoni, huku naye Yahaya Mudathir akianza badala ya Mhaiti, Leonel Saint-Preux.
Mabadiliko haya ya kikosi yanaashiria kuwa Azam ni timu yenye wachezaji wengi waliotayari kufanya kazi kwa kiwango kile kile.
Haikuwa rahisi kuona pengo la Mwadini Ali langoni, Manula alicheza vizuri, hali kadhalika Gadiel aliendelea kuwa katika ubora wake na kusababisha Erasto Nyoni asahaulike kwa muda.
Bado Azam ni timu bora na inaweza kufanya vizuri msimu huu, ingawa changamoto ni kubwa kwasababu timu kama Simba, Yanga zinaonekana kuwa na mipango thabiti ya kuchukua ubingwa.
Yanga sc walikuwa katika ubora hapo jana, lakini kilichowagharimu ni kukosa umakini kuzuia mipira mirefu iliyokuwa ikipigwa na mabeki wa Mtibwa.
Mabao yote mawili yalitokana na mipira ya aina hiyo na kwa bahati mbaya, Kelvin Yondani na ‘Cannavaro’ waliendelea kuzembea na kufungwa kirahisi.
Yanga walitawala sehemu ya kiungo hasa baada ya Marcio Maximo kumtoa Oscar Joshua na kumuingiza Omega Seme na kumrudisha beki ya kushoto Mbuyu Twite.
Ubora wa Yanga ulionekana kuanzia mawinga na sehemu ya kiungo, lakini walishindwa kutumia nafasi walizotengeneza.
Baada ya kuona Yanga wametawala katikati, Maximo alimtoa Twite na kumuingiza Said Bahanuzi kwa lengo la kuongeza nguvu zaidi kwasabau Twite hakuwa na majukumu mazito uwanjani kwani Mtibwa walikuwa hawapandi mbele.
Yanga wakishambulia kwa muda mrefu,walijisahau na ndipo Mtibwa walitumia mpira mrefu na kushuhudia Ame Ali akifunga goli la pili akiwa katikati ya Yondani na Cannavaro.
Matokeo ya jana yaliendelea kudhihirisha kuwa timu bora inaweza kupoteza mechi. Lakini kiujumla kikosi cha Yanga kimeenea na kinaweza kufanya vizuri mechi zijazo.
Kupoteza mechi ya kwanza kumewapunguzia morali kwa mbali sana, lakini Maximo ana uwezo wa kuwaweka wachezaji sawa na wakaamini kuwa huo ndio mpira na wakarudi kufanya kazi.
Kocha huyu ni mshindani na ataweza kufanya vizuri katika mechi zijazo.
Lakini ugumu wa mechi ya jana, ni dalili tosha kwa Yanga na Simba kuwa, ugenini kutakuwa sehemu ngumu sana kuvuna pointi.
Timu nyingi zinaonekana kuwa na mipango ya kutumia faida ya kuwa nyumbani kusaka pointi tatu muhimu.
Bado ni mapema, acha tusubiri kuona nini kitatokea.
Jumapili njema!
No comments:
Post a Comment