Tuesday, September 23, 2014

PANCHA SUGU YA PAUL KIONGERA YAMKOSESHA MECHI YA WATANI WA JADI!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
IMEELEZWA kuwa mshambuliaji wa Simba sc, Mkenya Paul Kiongera Mungai leo amefanyiwa vipimo hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia kuumia goti katika sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union, jumapili iliyopita uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katika vipimo vya awali, Kiongera amebainika kuwa na majeruhi sugu ya goti kama ilivyowahi kuelezwa na mtandao huu siku za nyuma.
Kiongera anayekonga nyoyo za mashabiki wa Simba alitokea benchi katika dakika ya 67 dhidi ya Wagosi wa Kaya, lakini dakika mbili kabla ya mechi kuisha alitonesha goti lake kwa kugongana na kipa Shaaban Hassan Kado, hivyo kulazimika kumpisha Amri Kiemba.
Baada ya kuumia, Kiongera alionekana kubadilika katika lugha yake ya mwili ‘Body Language’ akionesha kuwa ameumia sana na hataweza kurudi uwanjani kirahisi.
Kabla ya kusajiliwa majira ya kiangazi mwaka huu, ripoti zilifafanua kuwa Kiongera ana majeruhi ya muda mrefu aliyopata wakati anacheza Kenya, lakini kutokana na Simba kukosa mfumo wa kupima afya za wachezaji kabla ya kuwasajili walijikuta wakimsainisha mkataba akiwa na ‘pancha’.
Imefahamika kuwa Kiongera anaweza kuwa nje ya uwanja kwa wiki sita au miezi miwili na litakuwa pigo kwa Wanamsimbazi wanaovutiwa na uchezaji wa Mkenya huyo.
Kwa maana hiyo Oktoba 12 mwaka huu kuna uwezekano mkubwa nyota huyo akautazama mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga akiwa jukwaani na kuwaacha mashabiki wa Simba wakisikitika.
Mbali na Kiongera, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ni majeruhi pia, wakati Haruna Chanongo aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Coastal Union anaweza kurudi uwanjani muda wowote.
Wakati huo huo, Kiungo wa ulinzi aliyekaa nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa, Jonas Mkude ameimarika kiasi cha kusubiri maamuzi ya kocha Patrick Phiri kumpanga katika mechi ijayo dhidi Polisi Morogoro, Septemba 27 mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Mkude hajawahi kucheza chini ya kocha Phiri wala kufanya mazoezi, kwahiyo Mzambia huyo ndiye mwenye maamuzi ya kumpanga au kumpa mazoezi maalumu ili kuimarika zaidi.
Mechi iliyopita, Piere Kwizera alicheza nafasi ya Mkude, lakini alionekana kutoimudu kwa asilimia kubwa na alikosa maamuzi sahihi hasa katika upigaji wa pasi.

Alikuwa anachelewa kuanzisha ‘Movement’ pale inapobidi na alikuwa anapiga pasi vizuri bila kukosea -kukosea, lakini nyingi hazikuwa na madhara kwa Coastal Union.

No comments:

Post a Comment