Kocha mkuu wa Simba sc, Mzambia Patrick Phiri (kulia)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
SIMBA SC inajiandaa kuchuana na Polisi Morogoro katika mechi ya raundi ya pili, ligi kuu soka Tanzania bara itakayopigwa jumamosi uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Timu hizo mbili zitakutana zikiwa na matokeo tofauti ya mechi za ufunguzi wikiendi iliyopita. Simba walitoka sare ya 2-2 na Coastal Union uwanja wa Taifa, wakati Polisi Moro walitandikwa 3-1 na mabingwa watetezi Azam fc katika uwanja wa Azam Complex.
Kocha Patrick Phiri hakuridhishwa na kiwango cha timu yake na kuamua kwenda Visiwani Zanzibar tena kuwepa kambi ya maandalizi.
Simba kwasasa inaandamwa na majeruhi wengi. Jana kipa namba moja Ivo Mapunda alivunjika kidole mazoezini na atakaa nje ya uwanja kwa wiki nne.
Kuumia kwa Ivo ni pengo kwa kocha wa Simba ingawa ataweza kumtumia kipa bora wa msimu uliopita, Hussein Sharif ‘Casillas’.
Mbali na Ivo, Mkenya Paul Kiongera naye ataikosa mechi ya jumamosi. Bahati mbaya zaidi hata mechi ya watani wa jadi Oktoba 12 mwaka huu atakosekana kutonana na majeruhi sugu ya goti ambayo itamuweka nje ya uwanja kwa takribani wiki sita au miezi miwili.
Mshambuliaji Elius Maguli naye alikuwa anasumbuliwa na majeruhi, lakini kwasasa anaendelea vizuri na anaweza kucheza jumamosi.
Amerudi?: Gerard Jonas Mkude amesumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu
Kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude naye anaendelea kuimarika baada ya kukaa nje ya uwanjwa kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeruhi, lakini hajawahi kucheza chini ya Phiri. Kwa mazingira hayo dhahiri kiungo huyu anahitaji kupata muda wa kurudisha kiwango chake.
Nyota mwingine, Haruna Chanongo atakaa nje ya uwanja kwa siku 10 baada ya kuumia wikiendi iliyopita dhidi ya Coastal Union.
Beki wa kushoto, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ naye ana majeruhi, hivyo hana uhakika wa kucheza mechi ijayo.
Kutokana na majeruhi yanayoiandama Simba, kocha Phiri analazimika kufanya mabadiliko ya kikosi chake.
Ukiangalia kwa umakini unagundua kwa haraka kuwa baadhi ya wachezaji walioumia ni wa kikosi cha kwanza, hivyo itaathiri timu kwa kiasi fulani.
Mchezaji wa kikosi cha kwanza ndiye chaguo la kwanza kwa kocha. Inapotokea tatizo, analazimika kumpanga mbadala wake.
Ivo ni kipa namba moja, Casillas ni kipa namba mbili. Phiri anapomkosa Ivo, analazimika kumtumia Casillas.
Lakini kama Ivo yuko fiti kwa asilimia 100, Mzambia huyo hawezi kumuanzisha Casillas kirahisi.
Pengo?: Kipa Ivo Mapunda (kushoto) akisalimiana na waamuzi kwenye moja ya mechi ya Simba msimu uliopita
Nafasi ya Kiongera ina wachezaji wengi. Bado kuna watu kama Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, Elius Maguli na Amri Kiemba ambao wanaweza kuziba nafasi yake.
Safu ya ushambuliaji, Simba ina wachezaji wengi wanaofanana majukumu, hivyo ni rahisi mwalimu kubadilisha kikosi chake.
Kukosekana kwa Chanongo, Ibrahim Twaha anaweza kupata nafasi ya kucheza, lakini bado utakuwa mpango B wa Phiri. Asingeweza kumchezesha Twaha wakati Chanongo yupo.
Pengo la Mkude, bado ni gumu kuliziba, Piere Kwizera ameshindwa kukaribia uwezo wa kiungo huyo kijana.
Mechi iliyopita, Kwizera alijitahidi kupiga pasi sahihi, lakini nyingi hazikwenda maeneo sahihi. Alikuwa pole pole kuanzisha mashambulizi pale inapotakiwa na tatizo lilionekana wazi tofauti ambavyo angecheza Mkude.
Simba wanakwenda kucheza na Polisi Morogoro, kikosi kina majeruhi wengi, lakini wanaweza kupata matokeo kama watajipanga vizuri.
Majeruhi ni suala la kawaida katika soka, lakini athari yake ni kubwa na tunaona duniani kote timu zinavyohangaika pale zipoandamwa na tatizo hilo.
Kutumia wachezaji wa mpango B huwa kuna madhara kiufundi. Tumeona hata makocha wa Ulaya kama Arsene Wenger wanavyolalamika wanapokuwa na majeruhi wengi kikosini.
Mchezaji wa ‘Plan B’ huwa halingani na mchezaji wa ‘Plan A’. Siku zote ‘Plan B’ huwa inafanywa kwa kulazimisha kwasababu hakuna jinsi.
Paul Kiongera ni majeruhi
Phiri bila shaka anafanya kazi kubwa ya kuwafanya wachezaji atakaowatumia wajiamini kwasababu itakuwa mechi ya presha kwao.
Wanahitaji kushinda ili kuendelea kuwajengea imani mashabiki wao. Kinachotakiwa ni kuwapanga wachezaji kisaikolojia na waamini wataweza.
Wachezaji wa Simba bila shaka wako fiti katika utimamu wa mwili, ufundi na mbinu, lakini suala la saikolojia linatakiwa kuangaliwa zaidi.
Kikubwa vijana wanatakiwa kukalishwa chini na kuwapa mbinu zaidi ili wajiamini.
Ugumu wa mechi unakuja kutokana na namna Polisi wanavyocheza. Walifungwa na Azam fc 3-1, lakini walionekana kuwa na hofu kubwa hususani kipindi cha kwanza.
Wachezaji wa Polisi Moro walionekana wazi kutokuwa makini, kutojiamini na wakawaruhusu Azam wacheza mpira katika eneo lao na kushambuliwa zaidi.
Kadri dakika zilivyokuwa zinasonga mbele, walionekana kubadilika na kujiamni. Kipindi cha pili walicheza vizuri, walishambulia na kupata goli moja. Haikuwa kazi rahisi kwao kwasababu walikutana na mabingwa watetezi.
Kocha Adolf Rishard ni mzoefu wa ligi kuu, lazima amewatuliza vijana wake na kuwafanya wajiamini zaidi.
Simba watakutana na upinzani kwasababu tayari Polisi Moro wamejua udhaifu wao, hivyo kocha Adolf ameendelea kuwafundisha nini cha kufanya.
Lakini uwanja wa Taifa utakuwa mgumu zaidi kwa Polisi kutokana na mazingira ya Simba kwa sasa. Timu imewavutia sana mashabiki wake, wanajitokeza kwa wingi, hivyo presha itakuwa kubwa kwa wachezaji wa Polisi.
Lakini kama Simba watawaacha wacheze mpira hususani dakika za mwanzo (20-30) na kushindwa kuwafunga, basi mechi itaweza kuwa ngumu kwao.
Mabao ya mapema huwa yanawaharibia wapinzani . Kama Polisi watafungwa mapema zaidi watashindwa kucheza mpira na itatakiwa kocha atumie maarifa kuwapanga upya, lakini wakikaza dakika 20-30 za mwanzo, wataongeza kujiamini na mechi itakuwa ngumu kwa Simba.
No comments:
Post a Comment