Monday, September 15, 2014

TUTENGENEZE KATIBA INAYOLENGA KUTATUA MATATIZO YA WANANCHI WETU KWA MIAKA 50 IJAYO. Prof:Mwandosya.


Mwandosya akizungumza 1
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Prof. Mark Mwandosya ameeleza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2055 Tanzania itakuwa imeachana na umaskini katika nchi ya uchumi wa kwanza endapo kutakuwa na dhamira ya dhati hususani kuwa kuandika Katiba yenye kuleta nafuu kwa watanzania kwani kila kitu kwa Waafrika kinawezekana pasipo kuwa na Wazungu.
 Prof. Mwandosya alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa katiba ndani ya Bunge Maalum, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na katiba itakayozingatia vipaumbele ambavyo vinaweza kumkwamua mwananchi wa kawaida kuondokana na umasikini na kuliinua Taifa kiuchumi.
 Mhe. Mwandosya amesema kuwa kuhusu changamoto na kero zinazohusu mambo ya Muungano, katiba imejaribu kuzizingatia karibia zote, huku akieleza kuwa hali ya Muungano ni imara na itaendelea kuwa imara.
 Ili kufanikisha nchi inapiga hatua baada ya kuwa na Katiba bora, Mhe. Mwandosya amefafanua kuwa, watumishi wote wa Umma hawana budi kuliletea tija Taifa hili kwa kuwa misingi imewekwa ndani ya rasimu ya katiba  na kusisitiza kuwa Mtumishi wa Umma sio mtawala na mambo yanayohusu miiko na maadili ya mtumishi huyo yenye kumtumikia mwananchi serikali Katiba imeweza kuyazungumzia.
 
“Tumezungumzia kuhusu rushwa ambaye ni adui wa haki, kwamba hili tulitambue katika Katiba ili katika Sheria likasimamiwe vilivyo na pia tumezungumzia pia wale wanaouhujumu uchumi”, alisema Mhe. Mwandosya.
 Kuhusu haki za vijana, Mhe. Mwandosya ameeleza kuwa katika Rasimu ya Katiba wamezungumzia juu ya haki za vijana, haki za walemavu, haki za wazee, pamoja na haki za watoto, huku akiwashangaa baadhi ya wajumbe walioko nje ya bunge hilo wanapotoa shutuma kuwa wanapoteza wakati kana kwamba hawazungumzii mambo yanayowahusu wananchi.
 “Nawaomba wananchi watusikilize na wayazingatie haya tunayoyasema”. Alisema Mhe. Mwandosya.
 Akizungumzia kuhusu Vyombo vya Usalama, amesema kuwa Katiba inawalinda na kuwatambua viongozi wa usalama, ambapo sheria inawapa haki hata baada ya kustaafu ili wakaweze kuishi maisha bora kwa kuchukua dhamana kubwa, hivyo kwa dhamana hiyo viongozi hao wanapostaafu wanatakiwa kujiepusha na masuala ya kisiasa kwasababu.
 “Usalama wa Taifa, Jeshi, Polisi, Magereza na Uhamiaji, hawa tunawatengezea mambo mazuri sana wanapostaafu, kwahiyo tafadhari sana mkishatoka tusaidieni, toeni ushauri lakini mkijiingiza katika siasa na mafaili yetu huku mmeyashika hamtutendei haki”, alisema Mhe. Mwandosya.
 Aidha, ameomba kuwepo na Randama kwani hiyo inaandikwa katika lugha ambayo mwananchi anaweza kuisoma tofauti na katiba kwani hiyo inaandikwa kwa lugha ya kisheria, kwahiyo amependekezo kuwepo na randama kwa ajili ya wananchi.
 Mwandosya ameongezea juu ya suala la amani kuwa ni jambo kubwa sana, amewananga watu wenye tabia ya kutaka wananchi kuandamana wakapigwe risasi hao ni watu wasioitakia mema nchi, hivyo amewaasa wananchi walipinge kwa nguvu zao zote kuhusu suala hilo.
 “Nina ushauri kwa viongozi wenye kutaka wananchi wakapigwe risasi na Polisi, naomba watangulie wao wajipige risasi, unapotaka kuwa Shujaa anzia kwanza wewe mwenyewe, usiwapeleke vijana ambao ni matumaini ya nchi yetu, ndugu zangu hili jambo siyo la busara hata kidogo na wananchi mnapokwenda kuandamana, vijana mseme mnaandamana kwa nini? Kwasababu gani? Na kwa misingi gani na kwasababu ya nani? Ukishajibu haya maswali kwakweli mtaona nchi yetu kuwa ni nzuri sana, nchi ya amani”, alisisitiza Mhe. Mwandosya. 

No comments:

Post a Comment