Friday, September 12, 2014

WATANZANIA WATAKIWA KUTODANGANYWA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA


PIX 1 (9)
Mjumbewa Bunge Maalum la Katiba ambayepia niMwenyekiti waVyamavya Siasa vinavyounda TCD, Mhe. John Cheyo. 
(Picha na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma)
 
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
 
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCD Mhe. John Cheyo amewataka Watanzania kutodanganywa kuhusiana na mchakato mzima wa kusaka Katiba Mpya.
 
Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Cheyo wakati alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha asubuhi cha Jambo kinachorushwa na Televisheni ya Shirika la Habari Tanzania (TBC).
 
Mhe. Cheyo amesema kuwa ni vema viongozi kuacha kusema uwogo na kuwa waungwana katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya kwani si vema kuitakia Tanzania mabaya bali ni kutaka mchakato huo wa Katiba uendelee kwa amani.
 
Ameongeza kuwa Taifa la Tanzania linahitaji kuwa Taifa lenye nguvu kwani amani haiwezu kuwekewa thamani kwa vurugu, hivyo ametaka amani iliyopo nchini ilindwe na kuepuka kudanganywa na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema na nchi.
 
Mhe. Cheyo ameshangazwa kwa kitendo cha viongozi wa UKAWA kutoweka ajenda ya kurudi ndani ya Bunge hilo wala kuzungumzia kuhusu suala hilo la kurudi ndani, bali wamekuwa wakitaka wajumbe wengine walioko ndani watoke kwa kusema kuwa bunge hilo sio halali.
 
“Nawashangaa UKAWA kwa kutoweka ajenda ya kurudi ndani ya Bunge hili Maalum la Katiba na badala yake wao wanaweka ajenda ya kutoka ndani ya bunge hili tena kwa nguvu”, alisema Mhe. Cheyo.
 
Aidha, Mhe. Cheyo amewataka vijana nchini wawe na mshikamano na kuepuka kudanganywa na viongozi kwa kuambiwa mambo yenye uwongo huku akisisitiza kuwa Rais aliyeko sasa hivi ana nia njema ya kuipatia nchi Katiba iliyo bora na yenye kumfaa kila Mtanzania.
 
“Vijana achene kuvunjika miguu yenu bure, achene kukimbia kimbia barabarani huku mkilishwa maneno yenye uongo kuhusiana na mchakato huu wa Katiba, vunjikeni miguu kwa kufanya kazi kwa bidiii na sio kusikiliza uwongo”, alisema Mhe. Cheyo.
Akizungumzia kuhusu TCD, Mhe. Cheyo amefafanua kuwa TCD ni Jukwaa la majadiliano kwa ajili ya maridhiano na mapatano pale panapokuwa na tofauti kati ya vyama vya siasa.
 
“TCD ni Jukwaa kwa ajili ya kufanya majadiliano na si vinginevyo, hii ni meza ya maridhiano na nawaambia kuwa huko mnapokwenda ni kuchepuka, rudini ndani kwenye njia kuu”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
 
Naye mjumbe wa Kamati namba Sita ya Bunge Malaam la Katiba Mhe. Steven Wasira amewaasa Watanzania kwa kusema kuwa, watu wanaosema kuwa Bunge limenyofoa baadhi ya mambo muhimu yanayohusu wananchi ni waongo na wenye nia ya kupotosha Umma wa Tanzania.
 
“Kuna watu wanasema kuwa Bunge Maalum la Katiba limenyofoa baadhi ya mambo muhimu yanayohusu wananchi huo ni uwongo, ni mambo gani hayo yaliyonyofolewa? kwasababu kuna mambo mengi yameongezwa na kuboreshwa katika mapendekezo kwa ajili ya makundi mbalimbali ndani ya hiyo Rasimu”, alisema Mhe. Wasira.
 
Mhe. Wasira ameongeza kuwa katika Bunge hilo kuna Ibara ya Rasimu ya Katiba na sio ibara za CCM, amewataka Watanzania nchini wafanya uchunguzi na kusikiliza kwa kuchambua ili kupata ukweli wa hayo.
 
“Sisi tuko tayari kuvaana na viongozi wowote kwani tunataka Watanzania wote waamini shughuli zifanywazo ndani ya bunge hili na waepuke kudanganywa”, alisema Mhe. Wasira.

No comments:

Post a Comment