Sunday, September 14, 2014

YANGA SC BADO MFUPA WA AZAM FC UNAWASUBIRI, KAZI NDIO KWANZA INAANZA!


Kikosi cha Yanga kilichoanza dhidi ya Azam fc jana uwanja wa Taifa katika mchezo wa Ngao ya Jamii. Yanga ilishinda 3-0

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

0712461976

AZAM FC wameendelea kuonewa na Yanga katika mechi za Ngao ya Jamii baada ya jana kufungwa mabao 3-0  na vijana wa Marcio Maximo uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mwaka jana katika mechi kama hiyo, bao pekee la Salum Telela liliwapa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi vijana hao wenye makazi yao kule Chamazi.
Mechi ya jana, Azam walitabiriwa kufanya vizuri zaidi ya Yanga na makocha wa timu hizo, Mcameroon, Joseph Marius Omog (Azam fc) na Marcio Maximo (Yanga) walianzisha vikosi vifuatavyo:
Young Africans: 1. Deo Munish "Dida", 2. Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4. Nadir Haroub "Cananavao" (C), 5.Kelvin Yondani, 6.Mbuyu Twite, 7.Said Juma "Makapu"/Hassan Dilunga, 8.Haruna Niyonzima/Hamis Kizza, 9.Geilson Santos "Jaja"/Hussein Javu, 10.Mrisho Ngasa/Omega Seme, 11.Nizar Khalfani/Saimon Msuva/
Azam FC: 1.Mwadini Ali, 2.Shomari Kapombe, 3.Erasto Nyoni/Gadiel Michael, 4.David Mwantika, 5.Agrrey Morrsi, 6.Kipre Balou, 7.Himid Mao/Kelvin Friday, 8.Salum Abubakar, 9.Didier Kavumbag, 10.Kipre Tchetche/Ismail Diara, 11.Leonel st.Pres/Khamis Mcha
Ukitazama wachezaji wote wa Yanga na Azam fc wana ubora wa hali ya juu.
Kabla ya mechi hiyo ya jana, mchana niliongea na wachezaji wa zamani wa klabu za Simba na Yanga ambao kwa sasa ni makocha na wachambuzi wa soka.
Moja ya wanandinga hao wa zamani niliopata fursa ya kuongea nao ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Seklojo Chambua, beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa na beki na kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Mayay Tembele.
 Kikosi cha Azam fc kilichoanza jana

Chambua alisema: “Kwangu mimi nafikiri itakuwa mechi moja nzuri na yenye kusisimua kwasababu ukiangalia timu zote mbili zimejiandaa vizuri zaidi, zina wachezaji wazuri, zina uwezo wa kifedha, kwahiyo namna ninavyoiangalia hii, itakuwa ya upinzani sana na itatoa picha ni timu ipi imejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu huu.”
 “Azam sasa hivi imeimarika, ilivyocheza Kagame kila mtu aliona kuwa timu imebadilika, natarajia mechi ngumu, lakini matokeo yatapatikana ndani  ya uwanja na si nje ya uwanja. Kiujumla itakuwa mechi nzuri sana”.
Kwa upande wa Mayay yeye alisema: ““Mimi nakwenda kuona nidhamu ya kiufundi kwa upande wa Yanga, kwasababu Azam ukiangalia kwenye karatasi, safu yao ya ushambuliaji nafikiri ni nzuri kuliko Yanga, lakini ukiangalia kwenye makaratasi.” Alisema Mayay.
“Ukiangalia mtu kama Kipre Herman Tchetche, uwepo wa Mhaiti Leonel Saint Prexu pamoja na Didier Kabumbagu ni hatari sana. Hawa ni washambuliaji watatu wanaoweza kufanya lolote na wakati wowote. Hata kama mwalimu (Omog) atawapanga wote au wawili, bado safu yao ni nzuri ukilinganisha na Yanga”.
Pawasa alisema: ““Ni mechi ambayo huwezi kuitabiri haraka, lakini ukiangalia takwimu na uzoefu, unaweza kuona Azam wapo katika nafasi nzuri, kwasababu timu yao imeweza kuelewana, juzi juzi ilikuwa katika mashindano ya Kagame. Kwahiyo tayari Azam imeshapata mfumo kwa vile mwalimu wao amekuwa na timu kwa muda mrefu.” Alisema Pawasa.
“Wasiwasi ni mabadiliko ya mfumo wa Yanga, lakini najua Maximo ni mwalimu anayeujua vizuri mpira wa Tanzania, Maximo ni mwalimu mshindani, kwahiyo naamini ana kikosi kizuri, lakini wasiwasi wangu ni timu kombinesheni.”
Vitu vya mjomba: Mrisho Ngassa (kushoto) akitafuta namna ya kumtoka Erasto Nyoni (kulia)

Ukiwafuatilia Pawasa, Mayay na Chambua na watu wengine niliopata nafasi ya kuzungumza nao, waliipa nafasi Azam kutoa changamoto kubwa, isipokuwa Chambua aliongea kwa tahadhari.
Chambua alikiri kuwa Azam ni wazuri, lakini hakuwapa nafasi ya kushinda moja kwa moja na alihitaji kusubiri matokeo ya uwanjani.
Wengine kwa asilimia kubwa waliamini Azam fc ilikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kushinda kuliko Yanga.
Hoja yao ya msingi ni jinsi Azam fc walivyokaa pamoja kwa muda mrefu. Kumbuka kocha Joseph Omog alikuja nchini baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu mwaka jana akirithi mikoba ya Muingereza aliyeachia ngazi, Stewart John Hall.
Mcameroon huyu amekuwa na timu kwa muda mrefu zaidi ya Marcio Maximo aliyetua nchini mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.
Kutokana na namna Omog alivyoiandaa timu yake kwa muda mrefu, akashiriki kombe la Kagame na kucheza vizuri, ingawa aliishia robo fainali, watu wengi waliamini timu yake ingefanya vizuri.
Wengi waliitazama Yanga dhidi ya Thika United, kiukweli haikucheza vizuri. Wengine waliiona ikicheza mechi za kawaida pale Loyola, wakadhani haina kitu.
Ngassa na Nyoni mambo yalipamba moto

Lakini jana walikuja kivingine, timu ilionekana kuwa imara kuanzia nyuma, kati mpaka mbele.
 Walicheza kwa kuelewana, hawakuwa na presha, walijilinda vizuri, walidhibiti katikati, wakapanga mashambulizi na kupata mabao matatu.
Yanga walistahili kushinda kwasababu kimbinu na kiufundi walikuwa wazuri zaidi ya Azam fc, lakini haimaanishi wana Lambalamba ni wabaya.
Usijaribu kuwabeza Azam fc kwasababu wamefungwa na Yanga. Kuna mambo mengi hutokea katika mpira.
Kama unakumbuka, Azam walicheza vizuri kipindi cha kwanza, walishambulia mara kadhaa, lakini washambuliaji wake, Didier Kavumbagu, Kipre Herman Tchetche, Leonel Saint-Prexu walishindwa kutumia nafasi.
Baada ya kufungwa bao la kwanza dakika ya 58 na Jaja, wachezaji wa Azam walionekana kuchanganyikiwa kwa kiasi fulani. Pengine hawakuwa na utayari wa kufungwa katika mechi yao kutokana na maandalizi waliyofanya.
Unapokwenda kwenye mechi ni lazima ujue kuna kufunga na kufungwa, lakini ukiingia na akili ya kufunga na ukafungwa, basi unakosa utayari wa kupokea matokeo na hatimaye unaweza kutoka katika mfumo wa uchezaji.
Azam walishindwa kujipanga kabisa pale walipofungwa bao la pili dakika ya 66. Timu ilionekana kutokuwa na mipango na hapo ndipo Yanga walionekana kuwa bora zaidi.
Lakini kiuhalisia, Azam bado wana kikosi kizuri na ni timu inayokubali changamoto.
Azam huwa hawakati tamaa, mara zote wanakubali kimpira na ndio maana kama uliwasikia viongozi wake jana, walisifu kiwango cha Yanga na kuwapa hongera kwa ushindi.
Timu hii ipo kimpira kama vile Marcio Maximo alivyo kimpira. Kabla ya mechi kocha huyu wa Brazil aliwasifu Azam na kusema anawaheshimu, hivyo ataingia kwa tahadhari kubwa.
Maximo hana tabia za Kiswahili za ‘ooooh! Azam hawatoki au Simba hawatoki, tutawageuza Azam kitoweo cha krismas’, Yeye anazungumza ‘football’.
Mwaka jana Yanga iliwafunga katika mechi ya Ngao ya Jamii, lakini wakawafunga Yanga 3-2 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu na mechi ya mzunguko wa pili wakalazimisha sare ya 1-1.
Bahati mbaya Azam wakawazidi kete kwenye mbio za ubingwa. Kuwashinda iwe changamoto ya kujipanga zaidi kwasababu Omog anawarudisha vijana darasani.
Jumatatu njema! 

No comments:

Post a Comment