Benjamin Sawe
Bagamoyo
Taasisi ya Sanaa Bagamoyo imeaswa kuendelea kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni ambayo yatakidhi mahitaji ya soko kwa nchi za Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Bw Makongoro Nyerere kwa niaba ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mh. Margaret Ntantongo Zziwa katika Ufunguzi wa Tamasha la 33 la sanaa na utamaduni wa Mtanzania lililofanyika katika Taasisi hiyo mjini Bagamoyo jana
Bwana Makongoro alisema Sanaa na Utamaduni vinaweza kutumiwa kuelezea masuala yote yanayomuhusu binadamu na mazingira yake hususani suala zima la utaliii
Alisema ni wakati mwafaka kwa jamii kuondokana na dhana ya kuona watalii ni wale wa kutoka nje ya nchi na kusahau kuwa wale wa ndani ambao kwa idadi kubwa ni wengi wa kuwezesha Serikali kukusanya maduhuli ya kutosha.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Bw. Michael Kadinde alisema sanaa hutumika kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na Utawala Bora, kuhifadhi mazingira, madahara ya rushwa katika jamii, namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na aina nyingine nyingi za utoaji elimu katika jamii.
Alitolea mfano wa sanaa ya ngoma, nyimbo, hadidhi simulizi, majigambo, uchoraji na sanaa nyingine nyingi za makabila mbalimbali vinaeleza utamaduni wa Mtanzania hivyo huwa kitambulisho cha jamii.
Bw. Kadinde alisema sanaa huonya na kutaadhalisha jamii juu ya mambo mabaya yanayoweza kuleta madahara katika jamii ikiwa ni pamoja na kuendekeza rushwa, Vijana au jamii nzima kuwa na tabia zisizokuwa na heshima .
Aliomba Bodi ya Utalii ya Tanzania mahali palipo na vituo vya Utalii viwatumie wahitimu wa TaSUBa kuanzisha vikundi vya sanaa ili watangaze utalii wa nchi ili na kuongeza mapato ya nchi na jamii kwa ujumla
Alisema kutoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki kuna changamoto zake ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji ambapo iliyopo haiwezi kubeba mzigo mzito wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa nchi za Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment