Monday, September 12, 2011

EWURA YASHUSHA TENA BEI YA MAFUTA


Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeendelea kushusha bei za mafuta, safari hii petroli katika Jiji la Dar es Salaam yatakuwa yakiuzwa kwa Sh2,031 katika kipindi cha wiki mbili zijazo ikilinganishwa na Sh2,070, bei ambayo iliishia kutumika jana.

Ewura imekuwa na utaratibu wa kukokotoa na kutoa bei elekezi ya mafuta kila baada ya wiki mbili na hiyo mpya itaanza kutumika leo.Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema katika mabadiliko hayo bei ya petroli imeshuka kwa Sh38.03 sawa na asilimia 1.84, dizeli Sh45.15 sawa na asilimia 2.26 na mafuta ya taa bei imeshuka kwa Sh46.15 sawa na asilimia 2.33.

Kutoka na mabadiliko hayo, bei ya dizeli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh1,954 ikilinganishwa na Sh1,999 na mafuta ya taa yatauzwa kwa ni Sh1,933 yakiwa yameshuka kutoka Sh1,980.“Bei za rejareja kwa aina zote za mafuta zimeshuka ikilinganishwa na bei zilizoanza kutumika kuanzia tarehe 29 Agosti, 2011 kwa viwango mbalimbali,” alisema Kaguo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kushuka kwa bei hizo ni matokeo ya matumizi ya kanuni mpya ya ukokotoaji iliyoanza kutumika rasmi Agosti Mosi, mwaka huu.

Kaguo alisema mabadiliko ya bei yametokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ambako Petroli imeshuka kwa asilimia 2.54, dizeli asilimia 3.78 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.50.

Hata hivyo, Kaguo alisema bei za mafuta katika soko la ndani zingeshuka zaidi iwapo thamani ya Shilingi ya Tanzania isingeendelea kushuka dhidi ya Dola ya Marekani ambayo hutumika kununulia bidhaa za mafuta kutoka soko la dunia. Alifafanua kuwa katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na Dola.

Faida za kanuni mpya za ukokotoaji
Akizungumzia faida ya matumizi ya kanuni mpya, Kaguo alisema bei za rejareja zingepanda zaidi endapo kanuni ya zamani ingeendelea kutumika.“Kama tungeendelea na mwendo ule, badala ya kushuka hadi Sh2,031 kwa petroli, bei hiyo ingepanda hadi kufikia Sh2,205 na dizeli ingepanda hadi kufikia Sh2,126 badala ya Sh1,954 wakati mafuta ya taa bei yake ingepanda hadi kufikia Sh2,108 badala ya Sh1,933,” alisema.

Agosti 2, mwaka huu Ewura ilitangaza kushusha bei ya mafuta ambayo petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli ilishuka kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yalishuka bei kwa Sh181.37, sawa na asilimia 8.70.

Uamuzi huo uliibua mvutano kati ya wamiliki wa kampuni za mafuta na Serikali baada ya wafanyabiashara hao kugoma kuuza nishati hiyo muhimu.Lakini Agosti 10, mwaka huu Serikali ilitoa saa 24 kwa kampuni hizo za mafuta kurejea kutoa huduma hiyo mara moja na bila masharti huku ikizitaka kujieleza ni kwa nini zisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka agizo halali la Serikali.

Ewura baadaye ilitoa onyo kwa kampuni zilizogoma za Engen, Camel Oil, Oilcom na BP. Kampuni tatu zilitii agizo hilo isipokuwa BP ambayo iligoma hatua ambayo ilisababisha mkurugenzi wake mkuu kushtakiwa kwa kutotii amri hiyo.

Siku kumi na moja baada ya kushusha bei hizo, Ewura ilipandisha tena bei kwa kile ilichoeleza kuwa ni kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia kabla ya kushusha bei hizo wiki mbili zilizopita hadi kuishia jana

No comments:

Post a Comment