Saturday, September 24, 2011

TWANGA PEPETA KUSHAMBULIA TAMASHA LA 30 LA SANAA NA UTAMDUNI BAGAMOYO


Bendi maarufu ya African stars "twanga pepeta" inatarajia kufanya onesho katika tamasha la 30 la sanaa na utamaduni la Bagamoyo siku ya Jumatatu tarehe 26.09.2011 ndani ya ukumbi wa Tasuba  mjini Bagamoyo lifanyikapo tamasha hilo kila mwaka .

Kwa mujibu wa mmoja wa waandaji wa onesho hilo bw.Albert kawogo onesho hilo ni maalumu kwa ajili ya miaka 30 ya tamasha hilo ikiwa sambamba na uadhimishaji wa miaka 50 ya uhuru ambayo katika mkoa wa Pwani  inafanyikia mjini  Bagamoyo.

Kawogo aliongeza kuwa onesho hilo la aina yake lilopewa jina la Twanga na Tamasha litakuwa pia linawapa nafasi wakazi wa Bagamoyo na viunga vyake kuzitambua nyimbo mpya za albamu ya Twanga pepeta inayotarajiwa kutambulishwa baadae mwaka huu baada ya albamu ya Mwanadaressalaam.

Onesho hili la kihistoria ndani ya tamasha linafananishwa na onesho lililofanywa kwa mara ya mwisho na iliyokuwa bendi mashuhuri ya Diamond Sound lililofanyika mwaka 2008. Kiingilio katika onesho hili kinatarajiwa kuwa  5000/= na litaanza saa 3:00 usiku.

Ninawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ushuhudia onesho hili la aina yake katika historia ya tamasha alisema Kawogo.

Twanga pepeta inaendelea kutawala tasnia ya muziki wa dansi ikiwa na waimbaji mahiri kama Muumini Mwinjuma,Charles Baba,Luiza Mbutu na wacheza shoo wakali kama Asha Sharapova, Lilian Internet na Maria Salome.


No comments:

Post a Comment