Monday, September 26, 2011

Mke wa Rais Kikwete awataka wanafunzi kutojiingiza katika Mapenzi



Na Anna Nkinda – Maelezo
26/09/2011 Wanafunzi nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kujiingiza katika mapenzi wakiwa  masomoni kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanahatarisha maisha yao kwa kupata maambukizi ya Virusi vinavyosababisha Ugonjwa wa Ukimwi na ujauzito.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Barbro Johansson iliyopo Luguruni jijini Dar es Salaam kwenye  sherehe za mahafali ya kidato cha nne na cha sita.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwaambia wanafunzi hao kuwa elimu wanayoipata  itafungua maisha yao na ya jamii nzima. Itawapa njia ya kuwa na uwezo kiuchumi, itawajengea uwezo wa kujiamini na  kuweza kupaza sauti zao na kusikika kwani watakuwa na upeo mkubwa wa kuchambua mambo na kutoa maamuzi ya busara katika maisha.
 “Ninafahamu kwamba walimu, wazazi na walezi wamekuwa wakiwausia na kuwapa miongozo katika maisha yenu ya kutafuta elimu. Jambo ambalo ningependa muendelee kulizingatia kwa makini ni kwamba elimu mliyoipata bado ni mwanzo tu, hasa ukizingatia kukua kwa utandawazi.
Siku hizi mabadiliko ni ya haraka mno na yanamgusa kila mtu katika kila nyanja ya maisha. Ni vizuri mkajua kwamba ni wajibu wenu kuendelea kujifunza mbinu mpya za kuyakabili mabadiliko haya”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kuchukua tahadhari dhidi  ya ugonjwa wa Ukimwi kwani elimu waliyonayo  haitakuwa na maana kama wataruhusu kuambukizwa ugonjwa huo na kupata ujauzito ambao utawafanya wakatize masomo yao na hivyo kutotimiza ndoto zao

No comments:

Post a Comment