Mshambuliaji wa Yanga, Davis Mwape (kulia) akiwania mpira dhidi ya beki wa Mtibwa Sugar, Salum Sued wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Yanga jana kwa mara ya kwanza walivaa jezi za mdhamini wa Ligi Kuu Vodacom, lakini zikiwa na alama nyeusi badala ya alama nyekundu. Picha na Juma Mtanda wa gazeti la mwananchi.
Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi Yanga wameendelea kung'ang'ania mkiani mwa Ligi Kuu huku mahasimu wao Simba wakipata ushindi wa tatu mfululizo kwenye ligi hiyo katika mechi zilizofanyika jana kwenye viwanja vya Jamhuri, Morogoro na Mkwakwani, Tanga.
Yanga walishuka kwenye Uwanja wa Jamhuri wakiwa na matumaini ya kupata pointi tatu, lakini walijikuta wakilazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar, wakati Gervas Kago alifunga bao lake la kwanza tangu aanze kuichezea Simba na kuiwezesha timu hiyo kuilaza Villa Squad bao 1-0, huku Polisi Dodoma wakitoka suluhu na Ruvu Shooting.
Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi tisa na kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya kinara wa ligi JKT Ruvu kwa tofauti ya mabao.Mabingwa wa Kombe la Kagame Yanga waliokusanya pointi mbili katika michezo mitatu ya ligi waliyocheza mpaka sasa walilazimika kubaki ndani ya uwanja wa Jamhuri kwa dakika tano na kuondolewa na ulinzi mkali wa polisi FFU baada ya mashabiki wao wenye hasira kuanza kurushia mawe basi lililobeba wachezaji hao.
Kocha Sam Timbe akizungumzia pambano hilo alisema vijana wake walishindwa kutumia nafasi walizopata kwenye mchezo huo.
Mkenya Tom Olaba aliyeiwezesha Mtibwa Sugar kufikisha pointi nane mpaka sasa aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutawala sehemu ya kiungo, lakini walipoteza nafasi chake walizopata.Mtibwa ilianza mchezo huo kwa kasi na katika dakika ya 17, kipa Yaw Berko alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Said Mkopi.
Yanga ikicheza bila ya nahodha wake, Shadrack Nsajigwa ilionekana kupwaya katika kiungo na kuruhusu mashambulizi mengi golini kwake shukrani kwa juhudi binafsi za kipa Berko.
Mshambuliaji Thomas Mourice wa Mtibwa Sugar alipoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 40 kwa kushindwa kuunganisha vema krosi ya upande wa kushoto iliyopigwa na Said Bahanunzi.
Washambuliaji wa Yanga, Davis Mwape na Jerryson Tegete walikosa mabao katika dakika ya 29 na 42 waliposhindwa kutumia nafasi zilizotengenezwa na winga Julius Mrope.
Shujaa wa Ngao ya Jamii mshambuliaji wa Ghana, Kenneth Asamoah alishindwa kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Rashid Gumbo na kutemwa na kipa Munishi katika dakika ya 70.
Tanga; Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba wamedhamiria kurudia rekodi yao ya msimu wa 2009/10 waliotwaa ubingwa bila ya kupoteza mchezo wowote baada ya kuichapa Villa Squad bao 1-0.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kago alifunga bao lake la kwanza Ligi Kuu ya Tanzania katika dakika ya 7 akipokea krosi ya Haruna Moshi na kuipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Villa Squad.
Katika mchezo huo beki Victor Costa alifanya kazi ya ziada kuokoa bao lililotaka kufungwa na Mohamed Kijuso katika dakika za mwisho kwa mpira wa kichwa uliompotea kipa Juma Kaseja.
Pia winga wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alipewa kadi ya njano kwa kujiangusha kwenye eneo la penalti, huku Amri Ramadhan wa Villa Squad akipewa kadi ya njano kwa kuushika mpira kwa makusudi.
Dodoma; Polisi Dodoma wakiwa nyumbani kwenye uwanja wa Jamhuri walilazimishwa suluhu na Ruvu Shooting.
Wenyeji Polisi walitawala vizuri kipindi cha kwanza na washambuliaji wake, Bantu Admin na Kulwa Mobby kulifikia goli la Ruvu mara kadhaa, lakini kipa Benjamin Haule wa Ruvu Shooting alikuwa kikwazo kwao.
Shooting waliamka na kujibu mapigo kwa kushambulia kwa kushtukiza kupitia kwa washambuliaji wake Abdalah Juma na Abrahman Musa.
VIKOSI
Yanga: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Bakari Mbegu, Chacha Marwa, Nurdin Bakari, Julius Mrope, Rashid Gumbo, Jerryson Tegete (Kenneth Asamoah), Davis Mwape, Kigi Makassi (Idrissa Rashid).
Mtibwa Sugar: Deogartius Munishi, Juma Abdul, Issa Rashid, Salvatory Ntebe, Salum Sued, Shabaan Nditi, Said Mkopi, Masoud Ali, Said Bahanunzi, Thomas Mourice na Ali Mohamed.
Simba: Juma Kaseja, Nasoro Chollo, Amir Maftah, Juma Nyoso, Victor Costa, Jerry Santo, Shija Mkina, Amri Kiemba, Gervas Kago, Haruna Moshi na Ulimboka Mwakingwe.
Villa Squad: Abbas Nassoro, Haruna Shamte, Yassin Majota, Shai Mpala, Menard Mbugunza, Zuberi Dadi, Lameck Mbonde, Mussa Nampaka, Mohamed Kijuso, Mohamed Binslum na Nsa Job.
No comments:
Post a Comment