Monday, September 5, 2011

VODACOM TANZANIA YAPATA MKURUGENZI MTENDAJI MPYA

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom leo imemtangaza Rene Meza kuwa Mkurugenzi
Mtendaji mpya wa kampuni hiyo hapa nchini.

Rene ambae kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Bharti Airtel Kenya ana uzoefu mpana wa kimataifa katika sekta ya mawasiliano ya simu wa zaidi ya miaka kumi na miwili akiwa ameshafanya kazi barani Afrika, Asia na Larin-Amerika.

Akizungumzia uteuzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Johan Dennelind amesema:

“Tunayo furaha kubwa kwa Rene kujiunga nasi. Rene analeta uzoefu mpana kutoka nchi
alizowahi kufanyia kazi ikiwemo Paraguay, Pakistan na Kenya na amewahi pia kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Millicom’s (Tigo) nchini Tanzania hivyo basi ni wazi majukumu yake mapya katika Vodacom hayatokuwa na ugumu na atayamudu ndani ya muda mfupi.”

Rene anachukua nafasi ya Dietlof Mare ambae ameomba kupangiwa kazi nyengine baada ya kuwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne na nusu na hilo linafanyika kama sehemu ya programu ya Vodacom ya maendeleo ya uongozi. Taarifa ya kazi mpya atakayopangiwa itatolewa baadae.

“Napenda kumshukuru Dietlof,chini ya uongozi wake Vodacom Tanzania imepiga hatua kubwa, kwa sasa ni kampuni ya pili kwa ukubwa Afrika ikiwa na wateja zaidi ya milioni tisa ukiacha Vodacom Afrika Kusini. Amekuwa ni kiongozi wa kuhusudiwa na wengine, uendeshwaji wa huduma ya M-Pesa na nyengine zilizobuniwa na kusimamiwa nae zinaiweka Vodacom mahala pazuri kibiashara katika siku za usoni.”Alisema Dennelind.

Dennilend amesema Vodacom itautumia ujuzi wa Dietlof popote katika kundi la makampuni ya Vodacom.
Imetolewa na:

Mwamvita Makamba
Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano

Vodacom Tanzania

No comments:

Post a Comment