Thursday, September 22, 2011

YANGA ,AZAM SAFI SIMBA YAVUTWA MKIA

Mshambuliaji wa Yanga, Kenneth Asamoah (kushoto) akijaribu kuwatoka mabeki wa Villa Squad wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja Azam Chamanzi jijini Dar es Salaam.Yanga ilishinda 3-2. Picha na Jackson Odoyo.
Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi Yanga wamewanyuka Villa Squad pungufu kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Chamazi huku vinara wa ligi Simba wakilazimisha sare ya 3-3 na Toto African jijini Mwanza.Wakati Yanga wakipata ushindi wao wa pili na kufikisha pointi tisa, matajiri wa Chamazi, Azam wenyewe wamesogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo kwa kufikisha pointi 14 na kuisogelea Simba inayoongoza kwa pointi 15 baada ya kupata sare ya tatu katika mechi saba.

Macho ya wengi yalikuwa Uwanja wa Chamazi, ambapo Yanga ilipokuwa na kibarua kizito mbele Villa Squad waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia Nsa Job, lakini mabingwa hao walisawazisha kupitia Haruna Niyonzima na Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza waliongeza mabao mengine kabla ya Kigi Luseke kuifungia Villa bao la pili na kufanya matokeo kuwa 3-2.

Azam wenyewe wakiwa ugenini itabidi wamshukuru John Boko kwa kuwafungia bao pekee katika mechi dhidi ya Coastal Union akimalizia penalti yake iliyotemwa na kipa.

Katika mechi ya Yanga dhidi ya Villa, nyota wa kimataifa wa Yanga walilipa fadhila kwa kufunga mabao na kumpunguzia presha kocha wao Sam Timbe aliyepewa mechi tatu za kuhakikisha anapata ushindi.

Mshambuliaji Mwape alikosa bao katika dakika ya tano kwa kushindwa kuunganisha krosi ya Ally Shamte iliyotoka sentimita chache kutoka goli la Villa Squad.

Kenneth Asamoah naye alikosa bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua na kutoka nje, wakati nyota hao wa Yanga wakikosa Nsa Job alitumia vizuri mwanya wa kipa Yaw Berko kutoka kwenye mstali na kuinua mpira juu na kujaa wavuni katika dakika ya 11.

Dakika nne baadaye Niyonzima aliisawazishia Yanga bao kwa mpira wa adhabu ambao aliupiga na kwenda moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa 1-1.Kocha wa Villa Squad, Said Chamosi alimtoa Haruna Shamte katika dakika ya 24 na kumwingiza Evalist Maganga.

No comments:

Post a Comment