Thursday, September 22, 2011

Vodacom Mwanza Cycle Challenge kutimua vumbi mwezi ujao

Meneja udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania Rukia Mtingwa akionyesha nembo itakayotumika katika mashindano ya mbio za baiskeli "Vodacom Mwanza Cycle challenge 2011"zitakazoanzia Shinyanga hadi Jijini Mwanza mnamo tarehe 22 mwezi wa kumi mwaka huu.kulia Mwenyekiti wa chama cha baiskeli cha Mkoa wa shinyanga(Kamwashi) Elisha Eliasi.
  •  Washindi kuzoa zawadi kem kem
  • Makampuni mengine yajitokeze kudhamini mbio hizo
     Shinyanga Septemba 21 2011, Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza kuandaa na kuyadhamini mashindano ya baiskeli ya Vodacom Mwanza Cycle Challenge ambayo yamekuwa yenye mvuto wa hali ya juu katika mikoa ya kanda ya ziwa.Mashindano haya yataanzia mjini Shinyanga na kumalizikia Jijini Mwanza mwezi ujao na yatagharimu zaidi ya shilingi milioni 50.

Akizungumza naWaandishi wa Habari,leo/jana, katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi.

“Mashindano haya yameboreshwa kwa upande wa zawadi, ubora na viwango, na tofauti na miaka ya nyuma, mashindano ya mwaka huu yatahusisha mikoa miwili muhimu kwa mchezo wa baiskeli kanda ya Ziwa, yani Shinyanga na Mwanza”Alisema.

Alisema mashindano hayo yatafanyika tarehe 22 mwezi ujao na kwamba yatakuwa mbio za kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake, upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

“Washindi katika kila kundi watapewa zawadi mbalimbali ambazo tutazitangaza baadae,”Alisema.

Alifafanua kuwa mashindano ya mwaka huu ya Vodacom Mwanza Cycle Challenge yameandaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa takribani miaka mitano na pia Vodacom ina nia ya kuendelea kuandaa na kukuza mchezo huu ili Tanzania iweze kujulikana zaidi kimataifa katika mchezo huu wa baiskeli.


“Shindano hili la Vodacom Mwanza Cycle Challenge ni mahususi kwa kukuza mchezo huu hapa nchini kwa lengo la kupata wawakilishi bora katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,”alifafanua.

Katika kuzingatia kuwa mwaka huu Tanganyika inasherehekea miaka 50 ya uhuru, Vodacom Tanzania itatoa zawadi ya mshiriki mwenye umri wa kuanzia miaka 50 atakaemaliza wa kwanza katika kundi la washiriki 50 wa kwanza. Hivyo amewataka Watanzania wenye uwezo kujiandikisha kwa wingi ili kuweza kushiriki na hatimae kujishindia zawadi kem kem.

Nae Mwenyekiti wa Baiskeli Kanda ya Ziwa bwana Elisha Eliya, amesema mwaka huu ili kuleta mabadiliko na kuboresha zaidi mashindano haya, mbio zitaanzia Mkoa wa Shinyanga na kumalizikia Mwanza kwa sababu hii ni mikoa miwili inayoongoza katika uendeshaji wa baiskeli katika kanda hii.

Amewataka wanamichezo wote nchini wanaoshiriki katika mashindano haya kuanza kujiandaa wao pamoja na vifaa vyao vya michezo ili waweze kuwa katika hali nzuri ya kiushindani zaidi.
Ametoa wito kwa washiriki kutoka mikoa yote nchini kujiandikisha kwa wingi na kufika Shinyanga mapema ili kuhudhuria semina ya washiriki wote siku moja kabla ya mashindano.

Bwana Eliya amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani wa hali ya juu kwani njia itakuwa ya moja kwa moja na watahakikisha hakuna mtu atakaeingia kwenye mashindano kati kati ya njia hivyo kupata washindi halali,Na alichukua frusa hiyo kwa kutoa wito kwa makambuni mbalimbali hapa nchini kujitokeza kudhamini mbio hizo.


Vodacom Tanzania imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali kama vile Soka, Riadha, kuogelea, mashindano ya boti, mashindano ya Mbuzi, Vodacom Miss Tanzania, Tenisi na mingine mingi ili kuhakikisha kwamba taifa linafanya vizuri katika tasnia nzima ya michezo.

No comments:

Post a Comment